Sakata la Kikokotoo Lawaibua Tena CHADEMA....Tazama hapa Alichokisema Bulaya

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetaka suala la kikokotoo liwasilishwe bungeni na lijadiliwe kwa hati ya dharura ili iwe sheria itakayomnufaisha kila mstaafu.

Akizungumza na waandishi wa Habari katika ofisi za Makao makuu ya Chama hicho Waziri Kivuli ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira, Vijana na watu wenye Ulemavu Mh Ester Bulaya amesema pamoja na Rais wa Tanzania Dr John Magufuli kurudisha kikokotoo cha awali lakini bado haijawa sheria rasmi hali inayosababisha ubaguzi wa mafao kwa wastaafu.

Desemba 28, 2018 Rais Magufuli aliagiza kurejeshwa kwa utaratibu wa zamani wa wastaafu serikalini wa kupewa mafao ya mkupuo ya asilimia 50 badala ya asilimia 25 yaliyopendekezwa katika kanuni hizo mpya.

Akizungumza na waandishi wa habari Bulaya ambaye ni mbunge wa Bunda (Chadema), amesema alichokifanya Rais ni kama kutoa huduma ya kwanza kwa majeruhi wa ajali na uamuzi wake huo ukitungiwa sheria ni sawa na kutoa matibabu.

"Rais ametoa huduma ya kwanza kwa mgonjwa sasa anahitaji matibabu ili asife. Serikali inapaswa kupeleka bungeni marekebisho ya sheria kwa hati ya dharura kwa ajili ya kipindi cha mpito, isipofanyika hivyo hiki kitakuwa kicheko cha muda tu," amesema Bulaya.

Amesema sheria hiyo itatoa ufafanuzi wa mambo mengi kama fao la kujitoa lakini pia suala ambalo wafanyakazi walilalamikia la kuwa na uwakilishi mdogo katika bodi inayofanya uamuzi.

Bulaya amesema hatua kadhaa zinapaswa kuchukuliwa kuhusu suala la mafao ikiwamo Serikali kulipa madeni yake yote katika mifuko ya hifadhi za jamii, watumishi waliohusika na uwekezaji mbovu katika mifuko hiyo kuchukuliwa hatua.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad