Serikali imeagiza wavuvi wote waliokamatwa kwa kosa la kutohuisha leseni zao za Uvuvi na vyombo vyao kwa mwaka 2019, waachiwe na makosa yao yafutwe mara moja.
Hayo yamezungumzwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega,wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma.
Amesema kuwa Wizara yake juzi ilipata tarifa kutoka vyombo vya habari kwamba wavuvi katika ukanda wa Pwani bahari ya hindi hususani soko la feri Dar es saalam, hawakwenda kuvua samaki kwasababu ya kosa la kutokuwa na leseni za vyombo vyao na za uvuvi kwa mwaka 2019.
Kutokana na hali hiyo Ulega aliagiza kuwa wavuvi wote waliokamatwa kwa kosa hilo kote nchini kuachiwa mara moja kuendelea na shughuli zao huku akiwataka maafisa uvuvi kutoka katika ofisi zao na kuwafuata katika mialo mbalimbali ili kuwakatia leseni.
“Kwa kuzingatia kuwa hiki ni kipindi cha mwanzo wa mwaka ambapo leseni zinatolewa Wizara inaelekeza kwamba wavuvi wote waendelee kukatiwa leseni hadi Januri 31, 2019″amesisitiza Ulega.
Hata hivyo amewaagiza maafisa wote wa Wizara na Halmashauri katika kipindi hiki wawafuate wavuvi kwenye mialo ili kuwakatia leseni wenye sifa kulingana na sheria na kanuni za uvuvi.
Ulega amesema kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi inalojukumu la kuhakikisha kuwa rasilimali za uvuvi nchini zinasimamiwa, kuhifadhiwa na kuvunwa kwa kuzingatia sheria ili ziwe endelevu.
“Kazi hii inapaswa kufanyika kwa kushirikiana na Halmashauri nchini na wadau wa Uvuvi’alisema
Amesisitiza kuwa katika kutekeleza jukumu hilo Wizara imekuwa ikiendesha oparesheni dhidi ya Uvuvi haramu na biashara haramu ya samaki na mazao yake kwa takribani kipindi cha mwaka mzima.
“Shughuli za uvuvi zinatakiwa kutekelezwa kwa mujibu wa sheria ya uvuvi Na. 22 ya mwaka 2003 na kanuni zake za mwaka 2009 pamoja na sheria nyingine za nchi.
.