Serikali yazitaka kampuni za simu za mkononi kurudisha faida kwa jamii

Serikali yazitaka kampuni za simu za mkononi kurudisha faida kwa jamii
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye amezitaka kampuni za simu za mkononi nchini kurudisha faida kwa jamii ambayo ni wateja wake na wanatumia huduma za mawasiliano za kampuni zao

Nditiye ameyasema hayo wakati akikabidhi vifaa mbali mbali vya hospitali kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa ikiwemo vitanda, neti, mashuka na aproni vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni sita kwa niaba  Serikali kwa Hospitali ya Makole iliyopo Dodoma vilivyotolewa na kampuni ya simu za mkononi ya Halotel

“Nitoe wito kwa kampuni nyingine za simu za mkononi ziige mfano wa Halotel wa kurudisha shukrani kwa wananchi,” amesema Nditiye

Pia ameongeza kuwa mawasiliano ni moja ya Sekta ambayo inashika nafasi ya tano kwa maswali Bungeni ikiwemo Sekta nyingine za maji, afya, elimu, umeme, barabara ambapo Wabunge wamekuwa wakiuliza maswali mara kwa mara kuhusu Sekta ya Mawasiliano ambapo inadhihirisha kuwa wananchi wanatambua na kuthamini mchango wa mawasiliano katika maisha yao ya kila siku kwa kuwa mawasiliano ni uchumi na ni maendeleo

Vile vile amezitaka kampuni za simu za mkononi nne zilizosaini mkataba na kupewa ruzuku na Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) mwezi Desemba mwaka jana ikiwemo Vodacom, TIGO, Halotel na Shirika la Mawasiliano Tanzania kujenga minara  na kupeleka huduma za mawasiliano haraka kwa wananchi

Naye Mganga Mkuu wa Hospitali ya Makole, Dodoma Dkt. George Matiko akipokea misaada hiyo ameishukuru kampuni hiyo na kusema kuwa anaipongeza kwa kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli za kuboresha sekta ya afya kwa kujenga vituo vya afya nchi nzima na kuongeza fedha za kununua dawa, vitendanishi na vifaa tiba ambapo hadi sasa hospitali hiyo imepokea shilingi milioni 500 kutoka Serikalini ambapo zimewezesha ukarabati wa hospitali hiyo na kuongeza utoaji huduma kwa wanawake 2,000 waliojifungua na kufanya operesheni kwa wagonjwa 300

“Tunashukuru kwa jitihada zenu Halotel, mahitaji bado ni mengi, muendelee kutuunga mkono katika kuwahudumia wananchi,” amesisitiza Dkt. Matiko

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halotel, Tanzania Nguyen Van Son amesema kuwa wameamua kurudisha faida na kutoa shukrani kwa wananchi kwa kuwaunga mkono kwa kutumia huduma za kampuni yao ambayo imesambaa nchi nzima na inatoa huduma kwenye maeneo yote ya mijini na hasa vijijini

Nguyen ameishukuru Serikali kwa kuweka mazingira wezeshi na rafiki yaliyowavutia kuweza nchini kwenye Sekta ya Mawasiliano na wamedhamiria kuendelea kushirikiana na Serikali na wananchi kwa ujumla ili kupanua huduma za mawasiliano na kuhakikisha kuwa zinakuwa za viwango, ubora na gharama nafuu kwa mtumiaji

Katika hatua nyingine, Nditiye kwa niaba ya Serikali, ameshuhudia makabidhiano ya hundi ya shilingi milioni 20.6 baina ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilithi Mahenge na Nguyeni kwa ajili ya uanzishaji wa kiwanda cha kufyatua matofali cha kikundi cha vijana wa Dodoma ambapo makabidhiano hayo yamefanyika kwenye viwaja vya Barafu mjini humo

“Vijana wa Dodoma mtanufaika na Serikali kuhamia Dodoma, tumeona tuanzishe kikundi cha vijana ili waweze kuanzisha kiwanda cha kufyatua matofali na mradi huo utakuwa na vijana wa kutoka Jeshi la Kujenga Taifa ili wawasaidie ili baadae vijana waweze kuanzisha na kuendeleza viwanda vyao,” amesema Dkt. Mahenge

Pia, ametoa rai kwa vijana wajitokeze na kuchamkia fursa mbali mbali zilizopo mkoani humo na wasikubali kukaa bure, wajihusishe na shughuli za uzalishaji, wasikubali kukaa nyumbani na vijiweni

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad