Shafii Dauda Ampa Soma Haji Manara...Huwezi Kuwa Mkubwa Kuliko Simba..Heshimu Taasisi
1
January 27, 2019
Afisa habari wa Simba jana aliwajia juu mashabiki wa soka wanaomkalia kooni baada ya Simba kufungwa na Bandari kwenye mashindano ya SportPesa na kupoteza nafasi ya kucheza na Everton ambapo bingwa wa mashindano hayo hupata fursa hiyo.
Mashabiki wanalalamika Simba imefungwa halafu Manara anapost kuhusu Birthday yake pamoja na uzinduzi wa Perfume yake, Manara pia hakutumia busara kwa namna alivyowajibu mashabiki hao.
“Simba siyo baba yangu wala mama yangu. Yaani niahirishe jambo langu lakuniingizia kipato eti kwa sababu Simba imefungwa? Kudadeki”-Haji Manara, afisa habari Simba.
Manara kama afisa habari mipaka yake ni ipi?
Huu mjadala unasehemu pana sana, kwanza yeye mwenyewe ukimsikia namna anavyoongea alikuwa anawasilisha kwa njia ipi?
Kama unakumbuka siku za nyuma niliwahikusema hawa maafisa habari wa timu wana KPI’s zao kwa maana ya mipaka ambapo wanatakiwa waishie.
Lakini kwa sababu ya siasa za hivi vilabu wao wanakubali na kuruhusu mambo ya kijinga na ya hovyo ambayo yanakuwa yanafanyika wakati mwingine bila kujua madhara yake baadaye.
Ikafika mahali Manara akawa anajiona yeye ni mtu muhimu kuliko klabu kwa hiyo anaweza akaongea jambo lolote wakati wowote mahali popote na hakuna mtu anaweza kumgusa.
Sisi huwa tuna hoji, ile ni taasisi na yule ni msemaji wa taasisi. Msemaji wa taasisi anazungumza vitu rasmi kutoka kwa taasisi, klabu itaka kutoa taarifa kwenda kwa wanachama wao na mashabiki, wanampa msemaji wa timu.
Lakini kuna vitu ambavyo vipo nje ya mipaka ya msemaji wa timu Haji amekuwa akivizungumza kwa niaba ya klabu lakini viongozi wapo kimya maana yake ana baraka zote kutoka kwao.
Kwa mfano jana alikuwa anazungumza masuala ya Simba, alikuwa kwenye mkutano rasmi wa timu? Alikuwa klabuni? Majibu ni hapana, alikuwa kwenye mambo yake binafsi lajini amechanganya na mambo ya klabu si dhani kama ilikuwa ni mahala sahihi kuzungumzia mambo ya Simba.
Lazima tujue kutofautisha kati ya Haji Manara anapokuwa na mishe zake nyingine na anapokuwa kazini akiitumikia Simba.
Mimi nikiongea kama mkuu wa vipindi wa Clouds nitazungumzia mambo yanayohusiana na taasisi yangu katika muda na wakati mwafaka lakini naweza kuwa balozi au nawakilisha taasisi nyingine au kada nyingine. Nikiwa huko nitazungumzia jambo linalohusiana na taasisi ile siwezi kuwa pale nikaleta mambo ya Clouds kwenye hadhara ile ndio ninachokizungumza hapa.
Kwenda kufanya jambo jingine sio dhambi lakini kujua mipaka na hiki ndio nimekuwa nakizungumza siku zote, Haji mipaka yake inaishia wapi? Ukiwa msemaji unashambulia watu, viongozi na kuongea hovyohovyo? Hapana haiko hivyo.
Hao viongozi wengine ndio wanampampu wanaona kwamba anafanya sawa na hakuna tatizo kwa hiyo anapokuwa anafanya vitu vya kijinga halafu wao wanafurahia inabidi akifanya ujinga unaowaudhi basi wakubali pia.
Mara zote huwa nampongeza Haji kwa kuona fursa na kuitumia, katika hilo nipo na yeye hata wakati anazindua bidhaa zake mimi naunga mkono kwa asilimia zote.
Hakuna mtu aliyejuu ya taasisi yoyote!
Nakumbuka wakati Sir Alex Ferguson akiwa Manchester United kuna wakati ilitokea akina Beckham wanajiona wakubwa kuliko timu, Mzee Ferguson alimwambia wewe na umaarufu wako na kila kitu ulichonacho haitofika mahali ukawa mkubwa kuliko taasisi.
Nakubaliana na hii kauli ya Ferguson kwamba mtu hawezi kuwa mkubwa kuliko taasisi na huo ndio ukweli, taasisi itabaki kuwa mbele halafu watu ndio wanafuata. Ukilijua hilo utaheshimu na utajua mipaka na nafasi yako kwenye taasisi.
Mara nyingi ukimsikiliza Haji kwa makini kwenye maneno yake utagundua anazungumza kama mtu ambaye yupo juu ya taasisi jambo ambalo si kweli na sio kitu kizuri. Yeye pamoja na anachokifanya lazima abaki kwenye misingi ya kulinda taasisi, huwezi kuizungumzia taasisi kwa namna ile.
Mashabiki wana haki ya kumbana Manara kuhusu matokeo ya timu yao!
Haji anatengeneza matatizo halafu yanamrudia mwenyewe, kwa nini una-panic mashabiki wanapohoji kuhusu matokeo mabovu ya timu yao?
Wakati Simba inaanza kucheza michuano ya mabingwa Afrika walianisha malengo yao ambapo walisema, kufika hatua ya akundi ndio lengo kuu ambalo ni jambo zuri na kweli wamefika.
Baada ya kuingia hatua ya makundi, Manara aliwatangazia mashabiki wa Simba kwamba wanawania ubingwa sio dhambi, lakini kwa nini asingewaambia mashabiki ukweli kwamba tumefika hatua ya makundi lakini bado tupo kwenye kipindi cha mpito tunatengeneza Simba ambayo miaka michache mbele iwe kwenye level ya vilabu vingine vinavyofanya vizuri Afrika.
Kwa sasa baada ya kufanya mabadiliko ya mfumo tumefanikiwa kuingia hatua ya makundi, tunakwenda kushiriki kwa sababu tupo kwenye mashindano na tutashindana lakini kutokana na rasilimali tulizonazo na kikosi tulichonacho bado hatuwezi kushindana na vilabu kama Al Ahly na AS Vita pamoja na wengine lakini lazima tucheze. Mashabiki watakasirika kwa sababu umewaambia ukweli?
Sasa leo wanavyopigwa goli 5-0 halafu unakuja kutafuta huruma ya mashabiki wakati mwanzo uliwajaza na uliwaaminisha vingine, wakawa na matarajio makubwa kuliko uhalisia wenyewe hilo bomu linapolipuka linakuja kwako.
Simba hii mpya bado ipo kwenye mchakato wa kuelekea kule watu wanapotaka kuiona na matokeo chanya hayaji kwa kulala na kuamka. Tunatakiwa tuwaunge mkono katika kipindi hiki cha kuijenga Simba mpya na mashabiki wajue timu yao ipo katika hali gani hawawezi kulalamika.
Kuwa bingwa wa Afrika ni process ambayo haikamiliki kwa usiku mmoja, sio dhambi kuwaambia watu kwamba tumeingia hatua ya makundi tunakwenda kushindana lakini kiuhalisia hatupo katika nafasi ya kuwania ubingwa ambao ndio ukweli na huwezi kulazimisha kuwa unaenda kuwa bingwa.
Kwa mfano baada ya kufungwa na Bandari nilitegemea angewapongeza Bandari na kuwaambia mashabiki wa Simba kwamba walijiandaa kufika fainali na kushinda ili kupata fursa ya kucheza na Everton lakini wenzetu wamepata matokeo, hongera kwao tunawatakia fainali njema tunajipanga mwakani tukipata nafasi tutafanya vizuri tutakuwa tumeshajenga kikosi cha ushindani zaidi.
Kwa hiyo haji akubali hizo lawama za mashabiki asitoke povu ni vitu vya kawaida kwa sababu tayari alishawaahidi.
Shaffih Dauda on Sports Xtra (Clouds FM) January 26, 2019.
Tags
Shafii hamna chochote unacho jua shida ni kazi za kupeana Tumia muda mwingi kumshukuru ruge , unapaswa kuelewa kwamba si kila unacho sema ni sahihi na chambuzi una criticism , mnatumia muda mwingi wa kipindi kumjadili Haji na siyo kipindi , fanyeni habari za kitafi nendeni mkawaibue Wakina boko W apya
ReplyDelete