Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai ameeleza kwamba ni lazima Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali, Prof. Mussa Assad aweze kwenda kuhojiwa kwenye Kamati ya Maadili na asipokwenda atamuonyesha yupi ni bosi wake.
Akizungumza na vyombo vya habari leo, Spika Ndugai amesema kwamba CAG siyo muhimili kama jinsi ambavyo anakuzwa na baadhi ya watu na badala wake yeye ni Ofisa anayefanya kazi za kuchunguza kazi ambazo zilitakiwa zifanywe na wabunge.
Akizungumzia kuhusu kinga yaCAG, Ndugai amesema suala la maadili haliangalii kuhusu cheo hata akiwa yeye mwenyewe haruhusiwi kuizungumza vibaya nchi yake akiwa nchi nyingine kwani maadili hayaruhusu.
"Hata awe nani? msichanganye vitu, hii haina exception, ndiyo maana wanaoapishwa na Rais lazima wasome kiapo cha maadili. Ni maadili unatoka nje ya nyumba alafu unaanza kwamba ooh mke wangu mimi.....kuna madili hapo?. Ni maadili atakuja tu na litaisha" Amesema Ndugai na kuongeza;
“Kuna rafiki yengu mmoja yupo Uganda , kule Uganda CAG ni Ofisa wa Bunge,na Ofisa wa Bunge anaweza kumgomea Spika? Mihimili iko mitatu na niwahakikishie CAG hiyo tarehe 21 atakuja tu.
“Wengi ambao wanaongea kuhusu hili najua wanatoka upande gani,wapinzani wengi wao wanawaza kupinga tu.
“Huwezi kutoka hapa halafu unakwenda kuisema nchi vibaya.Kazi yetu sote ni kuhakikisha nchi inakaa vizuri”
Katika hatua nyingine, Spika Ndugai amesema mbunge anayempa shida pale anapotaka kumwadhibu ni Zitto Kabwe.
Ndugai amesema amekuwa akichelea kumfukuza bungeni mbunge huyo wa Kigoma Mjini kwa kuwa ndiye pekee anayewakilisha Chama cha ACT-Wazalendo.
"Unajua niseme ukweli, huyu mbunge amekuwa akinipa tabu sana, ananipa tabu sababu ndio mbunge mmoja wa chama chake,” amesema Ndugai.
“Hawa wengine huwa nafukuza sababu wenzao wapo, sasa huyu (Zitto) ni mmoja tu wa chama chake (ACT Wazalendo).”
Ndugai ametoa kauli hiyo wakati akijibu swali kuhusu kauli za Zitto Kabwe kuhusu kauli ya Ndugai kuwa Bunge halifanyi kazi kwa muda na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kutokana na kuitwa kuhojiwa na Kamati ya Maadili, Haki na Madaraka ya Bunge.
Msingi wa kauli hiyo ulitokana na ufafanuzi wa Ndugai kuhusu nguvu ya Bunge kumuita CAG Assad, akisema Zitto amekuwa akipotosha ukweli wa jambo hilo.
”Hivyo naamua kumuacha tu kwa kutumia busara lakini ukweli huko mbele ya safari nitachoka na nitamchukulia hatua.Bungeni pale watu wanashindana kwa hoja na inaungwa mkono na wabunge wengine.
“Ndio maana wabunge wakiunga mkono wanne ujue hilo jambo linatupwa na Zitto anakwama kwasababu hana wa kumuunga mkono katika mambo yake.
Ameeleza kwa sasa wabunge wengine wako Dodoma wakiendelea na Kamati za Bunge lakini Zitto yupo Dar es Salaam anahangaika kwenye korido kuhusu kuupinga muswada wa vyama vya siasa.
”Muswada unaendelea kama kawaida, na ukifika Bungeni utapitishwa .Zitto alitakiwa kuwa kule ili atoe maoni yake ili yafanyiwe kazi,”amesema Spika.
Spika Ndugai Amshangaa Zitto Kabwe....Asisitiza CAG Ni Lazima Akahojiwe na Kamati ya Bunge
0
January 17, 2019
Tags