TAKUKURU yaomba kumchukua Malinzi na mwenzie wakahojiwe

TAKUKURU yaomba kumchukua Malinzi na mwenzie wakahojiwe
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imeomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kumchukua aliyekua Rais wa TFF Jamal Malinzi na Katibu wake, Mwesigwa Selestine kwa jailli ya kuhojiwa.

Wakili wa Takukuru,  Leonard Swai akisaidiana na Nickson Shayo ameiomba Mahakama hiyo jana Jumatano Januari 16, 2019 mbele ya hakimu mkazi mkuu, Wilbard Mashauri wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.

Malinzi,  Selestine pamoja na wenzao watatu wanakabiliwa na mashtaka 30 yakiwemo ya kula njama, kughushi na kutakatisha fedha katika kesi ya jinai namba 213/ 2017.

Swai aliieleza mahakama hiyo kuwa wanaomba kibali cha kwenda kuwahoji washtakiwa hao kwa mashtaka mengine tofauti na yanayowakabili Kisutu.

"Tunaiomba Mahakama yako itoe kibali cha kwenda kumhoji mshtakiwa wa kwanza na wa pili katika mashtaka mengine na sio haya yaliyopo mahakama hapa," alidai Swai.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mashauri alikubaliana na upande wa mashtaka na kuruhusu Malinzi na Selestine kwenda kuhojiwa  ili warejeshwe Januari 17, 2019.

Baada ya Hakimu kuruhusu washtakiwa hao kwenda kuhojiwa, wakili wa utetezi,  Richard Rweyongeza aliwataja mawakili watakaoambatana na washtakiwa kwenda kuhojiwa Takukuru kuwa ni  Kung'e Wabeya na Adolf Bunyoro.

Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 21, 2019 itakapoendelea na ushahidi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad