Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imetambulika kufikia ngazi ya tatu (Maturity Level 3) ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya ubora wa mfumo wa udhibiti wa dawa, hatua ambayo imeifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kupata mafanikio hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es salaam, kuhusu mafanikio ya taasisi hiyo katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Adam Fimbo, alisema kuwa TFDA imepata mafanikio hayo makubwa kutokana na kuwa na mifumo thabiti ya udhibiti wa ubora, usalama na ufanisi wa dawa, ambapo Desemba mwaka huu, imetambulika kufikia ngazi ya tatu (Maturity Level 3) ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya ubora wa mfumo wa udhibiti wa dawa, hatua ambayo imesaidia Tanzania kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kufikia hatua hiyo muhimu.
“Hii ni hatua kubwa kwa kuwa taasisi ya mfano barani Afrika katika udhibiti wa bidhaa za chakula, dawa, vipodozi, vifaa tiba na vitendanishi na hivyo kuvutia nchi mbalimbali kuja TFDA kujifunza mifumo iliyopo na kwenda kuitekeleza nchini mwao na sasa mifumo yetu imetambulika na kujulikana na nchi nyingi kwa mfano Zimbabwe, Rwanda, Kenya, Uganda, Ethiopia, Sudan Kusini, Botswana, Mauritius, Lesotho na Bangladesh” alisema Kaimu Mkurugenzi huyo wa TFDA
Sambamba na hilo, Kaimu Mkurugenzi huyo wa TFDA, aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano mfumo wa usajili wa bidhaa umeendelea kuimarika mwaka hadi mwaka ambapo idadi ya bidhaa za chakula, dawa, vipodozi, vifaa tiba na vitendanishi vilizosajiliwa imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka,
Akitolea mfano katika kipindi cha 2015/16 hadi 2017/18, TFDA imesajili jumla ya bidhaa 14,345 kutoka bidhaa 8,866 zilizokuwa zimesajiliwa mwaka 2015/16 ambapo ni sawa na ongezeko la 62%. Ikiwa ni kuongezeka kwa uelewa wa matakwa ya sheria miongoni mwa wafanyabiashara na kukua kwa biashara.
Kaimu Mkurugenzi huyo wa TFDA, alifafanua kuwa tathmini na usajili wa bidhaa hufanyika kwa lengo la kuhakiki endapo bidhaa zinakidhi vigezo vya usalama, ubora na ufanisi kabla ya kuruhusiwa katika soko. Kuwepo kwa bidhaa nyingi zilizosajiliwa katika soko ni uthibitisho kuwa walaji wanapata bidhaa zilizo salama, zenye ubora na ufanisi.
Kuhusu udhibiti wa uingizaji na usafirishaji wa bidhaa ndani na nje ya nchi, alisema kuwa katika kutekeleza hilo ambalo ni agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, la mwezi Mei, 2017, TFDA imeweka wakaguzi wake ambao hufanya kazi masaa 24 kwa siku zote za juma, pamoja na mfumo wa kieletroniki wa utoaji vibali vya kuingiza na kutoa nchini bidhaa unaomwezesha mteja kutuma maombi, kufanya malipo popote alipo na hatimaye kupata kibali ndani ya masaa 24.
Aidha, kwa kutumia mifumo hiyo, mwenendo wa utoaji wa vibali vya uingizaji na utoaji wa bidhaa nje ya nchi umeongezeka ambapo katika mwaka 2017/18, jumla ya vibali 11,866 sawa na ongezeko la 91% ukilinganisha na 13,018 mwaka 2016/17 vilitolewa.
Vilevile, katika jitihada za kujenga Tanzania ya viwanda ifikapo 2025, TFDA imeendelea kutoa msaada wa kiufundi na kuwajengea uwezo wenye viwanda vya dawa nchini na kushawishi wawekezaji kujenga viwanda vya dawa, chakula, vipodozi na vifaa tiba. Ambapo hadi sasa jumla ya wawekezaji 70 wameonesha nia ya kuanzisha viwanda vya dawa huku viwanda vinne vikiwa vimeanza kujengwa katika maeneo ya Morogoro na Kibaha.
Sambamba na hilo, Kaimu Mkurugenzi huyo alisema kuwa, mafanikio mengine ya TFDA yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitatau ya Serikali ya Awamu ya Tano ni pamoja na kuweka mifumo madhubuti ya ufuatiliaji wa madhara yatokanayo na matumizi ya chakula, dawa na vifaa tiba ili kuweza kutambua, kutathmini na kuzuia madhara yasiyovumilika yasitokee kwa wananchi.
Pia, kwa kipindi cha mwaka 2015/16 hadi 2017/18, matokeo ya uchunguzi wa sampuli yanaonesha kuwa bidhaa zilizochunguzwa zimekidhi viwango vya ubora na usalama kwa wastani wa 88%.
Alifafanua kuwa maabara ya uchunguzi wa dawa imekidhi vigezo vya kimataifa na kutambuliwa rasmi na Shirika la Afya Duniani (prequalification), maabara ya uchunguzi wa chakula na ile ya maikrobiolojia zimepata ithibati kwa kiwango cha kimataifa cha ISO/IEC 17025:2005. Hii inafanya majibu ya uchunguzi yanayotolewa na maabara kuaminika na hivyo kutambulika kitaifa na kimataifa, hali ambayo inamuhakikishia mwananchi uhakika wa maamuzi ya mamlaka kuhusiana na ubora wa bidhaa.
TFDA imefanikiwa kufikia na kuvuka malengo iliyojiwekea katika utekelezaji wa mipango kazi yake, ambapo katika kipindi cha mwaka 2017/18 itaendelea kutoa kipaumbele katika utekelezaji kwa ufanisi wa malengo mahususi nane (8) yaliyomo katika Mpango Mkakati mpya wa miaka mitano (5) yaani 2017/18 – 2021/22, ili kulinda afya ya jamii.
TFDA Yaongoza Afrika kwa kuwa na Mfumo Bora wa Udhibiti wa Dawa
0
January 01, 2019
Tags