Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa anatarajia kukutana na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un kwa mara ya pili katika hatua ya Washington kuendelea kutafuta mbinu za kuifanya Korea Kaskazini kuachana kabisa na silaha za nyuklia.
Trump amesema hivi karibuni alipokea barua "nzuri" kutoka kwa Kim Jong-un, akidai kuwa Marekani imepiga hatua kubwa katika mazungumzo na Pyongyang bila ya kueleza maudhui ya barua hiyo.
"Tulianzisha uhusiano mzuri sana, mambo mazuri yanayotokea," Trump aliwaambia waandishi wa habari katika White House.
"Tulifanya mkutano na Kim miezi sita iliyopita huko Singapore. Tunaweza kuwa na mkutano mwingine.Ningependa kukutana na vilevile yeye anataka kukutana."
Uamuzi huo umekuja siku chache baada ya hotuba ya kitaifa ya KimJong Un siku ya Jumanne ambapo alisema kuwa atakuwa tayari kufanya mkutano tena na Trump.
Hata hivyo Kim Jong Un ameonya kuwa Pyongyang inaweza kufuata "njia mpya" ikiwa Washington haitoondoa vikwazo vyake dhidi ya Korea Kaskazini.
Majadiliano kati ya Marekani na Korea ya Kaskazini yamekwama kutokana na shinikizo la kiuchumi lililowekwa na Marekani dhidi ya Korea Kaskazini.
Nchi hiyo imeitaka Washington kuondoa vikwazo dhidi ya nchi yake lakini Marekani imesisitiza ya kuwa itafanya hivyo pale tu silaha zote za nyuklia zitakapotokomezwa.
Trump apokea barua kutoka kwa kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un
0
January 04, 2019
Tags