BAADA ya kimya kirefu hatimaye kiungo wa Yanga, Papy Kabamba Tshishimbi amerejea klabuni huku chanzo cha kuchelewa kikiwekwa wazi. Tshishimbi raia wa DR Congo aliondoka Yanga mwishoni mwa mwaka jana na kurejea kwao ambapo alikuwa na matatizo ya kifamilia.
Hata hivyo licha ya kutua, alikuwa akifanya mazoezi binafsi na siyo ya timu ili kujiweka fiti kwa ajili ya mechi zinazofuata ukiitoa hii ya leo dhidi ya Stand United ambapo yeye hayupo kwenye msafara. Tshishimbi alijiunga na Yanga msimu msimu uliopita kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Mbabane Swallows ya Eswatini.
Chanzo makini kutoka ndani ya Yanga kinadai kuwa, Tshishimbi aliomba ruhusa kutokana na kukabiliwa na matatizo ya kifamilia lakini hata alipomaliza aligoma kurejea kwa wakati huku akiwafungia vioo mabosi wake akishinikiwa kulipwa fedha zake za usajili kabla ya kurejea nchini Jumanne iliyopita.
“Ngoja nikuambie jambo yaani haya yote unayoyaona sasa yamekuja baada ya Tshishimbi kuona ufalme wake unapungua ndani ya kikosi chetu, hasa baada ya kocha wetu Mwinyi Zahera kuondoa jicho la kumtegemea kama ilivyokuwa awali ambapo Yanga ilionekana haiwezi kucheza bila uwepo wake.
“Suala hili limemfanya aanze kudai malimbikizo yake huku akitishia kuondoka kwa madai ya mkataba wake kumalizika siku chache zijazo, ukweli ni kwamba tangu Tshishimbi alipougua ameshindwa kurejea katika kiwango chake hivyo inampa shida kuona Yanga inasajili viungo wengine ambao kwa namna fulani wanatishia uwepo wake,” kilisema chanzo hicho.
Championi lilimtafuta Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Yanga, Dismas Ten, ili aweze kuweka mzani sawa ambapo alisema: “Tshishimbi yupo nchini na alirudi kabla ya Makambo (Heritier), lakini hawezi kuungana na timu kwa sababu hajafanya mazoezi ya kutosha, hivyo yawezekana akaungana na timu katika michezo ijayo baada ya kurejea kutoka Shinyanga.
“Kuhusu madai ya kugoma mimi sijui zaidi ila ninachojua alikuwa kwenye matatizo kwao nchini DR Congo, ila mbali na hivyo pia hajaenda na timu Shinyanga kwa kuwa hajawa fiti na wenzake.”