Pia shirikisho hilo limesema litaendelea kuiunga mkono na kushirikiana na Serikali ya awamu ya tano pamoja na rais wake Dkt. John Magufuli na kwamba watahakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia masharti ya ajira zao.
Hayo yamesemwa jana (Jumatatu, Januari 7, 2019) na Katibu Mkuu wa TUCTA, Yahya Msigwa katika hotuba yake aliyoitoa kwa wafanyakazi baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kupokea maandamano ya amani ya vyama vya wafanyakazi.
Watumishi wa taasisi mbalimbali jana wameandamana jijini Dodoma katika viwanja vya Nyerere Squarekwa lengo la kumpongeza Rais Dkt. Magufuli kwa uamuzi wake kufuta kikotoo kipya cha mafao ya wafanyakazi kilichopendekezwa katika kanuni za sheria ya Mifuko ya jamii.
Katibu huyo wa TUCTA amesema mara nyingine makundi ya wanasiasa yamekuwa yakisema maneno ambayo wao hawajayasema jambo ambalo limekuwa likiwachonganisha na wadau wao wakiwemo wanachama pamoja na Serikali.
”Wafanyakazi wanaona fahari kwa sababu Rais Dkt. Magufuli anasikiliza kero mbalimbali zinazowakabili na kuzitatua kwa wakati. Aliposema atafufua Shirika la Ndege Tanzanzia amelifufua na sasa tuna ndege saba pamoja na ujenzi wa miradi mkubwa ya umeme, barabara ambayo yote inaenda kutengeneza ajira.”
Hata hivyo, ameiomba Serikali ifanye uchunguzi kwenye miradi inayotekelezwa na mifuko ya hifadhi ya jamii kwa sababu hawana uhakika kama miradi hiyo imerejesha fedha. Pia ameiomba Serikali iongeze mishahara kwa watumishi wa umma.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu amesema Serikali ipo tayari wakati wote kuyapatia ufumbuzi matatizo ya wafanyakazi ikiwa ni pamoja na kuboresha mishahara na maslahi yao. “Wito wa Serikali ni kuwa wafanyakazi watekeleze majukumu yao kwa uadilifu,weledi na kujituma ikiwa ndio chachu ya kufikia malengo na ustawi wa nchi yetu.”
Kuhusu suala la kupandisha mishahara, madaraja na maslahi ya wafanyakazi kwa ujumla, Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Magufuli alishalitolea maelekezo na kwamba Serikali inayafanyia kazi maelekezo yake, hivyo amewaomba wafanyakazi waendelee kuwa wavumilivu.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kulipa stahili za watumishi wa umma kwa wakati na kulipa madeni hatua kwa hatua, ambapo kati ya Julai 2018 hadi Septemba 2018, Serikali imelipa sh. bilioni 184.9 za madai mbalimbali ya watumishi.
“Kati ya kiasi hicho Serikali imelipa shilingi bilioni 49 kwa ajili ya malimbikizo ya mishahara kwa watumishi 28,214 ambayo yanajumuisha shilingi bilioni 19.2 walizolipwa walimu 16,214. Hata hivyo Serikali inaendelea na utafiti wa tathmini ya kazi katika wizara na taasisi mbalimbali ili kupanga vizuri mishahara na motisha kwa watumishi wa umma.”