Tume ya Uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inasema matokeo ya awali ya uchaguzi mkuu huenda yakachelewa na kupita tarehe iliyotarajiwa ya Januari 6.
Rais wa tume hiyo, Corneille Nangaa, amesema kituo kikuu cha kuhesabia kura bado kinasubiri matokeo ya zaidi ya asilimia 80 ya kura zilizopigwa kutoka vituo mbalimbali kote nchini humo.
Aidha amesema bado ni mapema mno kubaini chanzo cha kuchelewa kwa matokeo hayo, lakini vyama vya upinzani vinadai hiyo ni njama ya kuiba kura.
Wakati huo huo shirika la Umoja wa Afrika pamoja na Shirika la Kimaendeleo la Kusini mwa Afrika - SADC yametaja uchaguzi huo kama ulioendeshwa vizuri kwa kiwango kikubwa, licha ya kuwa na matatizo kadhaa ya kiufundi pamoja na machafuko katika baadhi ya maeneo.
Wameongezea kuwa wapiga kura hawakuelimishwa vizuri kuhusu utumizi wa vifaa vya kielektroniki vya kupigia kura ambavyo vimetumika kwa mara ya kwanza nchini humo.
Wakizungumzia changamoto za kuandaa uchaguzi katika maeneo yaliokuwa na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola na mapigano, Umoja wa Afrika ulishtumu hatua ya kuwafungia baadhi ya wapigaji kura kukamilisha haki yao ya kidemokrasia, huku wakisisitiza kwamba washikadau wa masuala ya kisiasa hawakushirikishwa katika uamuzi huo.
SADC pia wamekiri kwamba huu ndio uchaguzi wa kwanza wa kujitegemea kifedha nchini humo, ikiwa ni hatua muhimu kwa ukuaji wa kidemokrasia.
Shirika la Umoja wa Afrika linatumaini kuwa matokeo yataakisi uamuzi wa wananchi, na kuwataka wale ambao hawatokubaliana na matokeao hayo kufuata njia ya haki ya sheria kuupinga.