Tundu Lissu Aanza Ziara Barani Ulaya

Tundu Lissu Aanza Ziara Barani Ulaya
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu ameanza ziara barani Ulaya na leo atakuwa London, Uingereza ambako amesema ataeleza kwa kina kile alichoandika katika waraka aliotoa kwa ajili ya mwaka huu.

Ziara ya Lissu inaanza baada ya Desemba 31, mwaka jana kuhitimisha safari ya matibabu aliyoanza Septemba 7, 2017 baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana kwa zaidi ya risasi 30 mjini Dodoma muda mfupi baada ya kutoka kuhudhuria kikao cha mchana cha Bunge.

Akizungumza na  gazeti la Mwananchi jana, Lissu ambaye hivi karibuni ameeleza nia yake ya kugombea urais kupitia Chadema, alisema leo ataitikia mwaliko wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).

Lissu alikwenda Ubelgiji Januari 6 mwaka jana kuendelea na matibabu akitokea Hospitali ya Nairobi, Kenya na katika kipindi chote cha matibabu, amefanyiwa upasuaji mara 22.

Alisema baada ya kutoka Uingereza, amepata mwaliko mwingine wa kwenda katika ofisi za Umoja wa Ulaya (EU) zilizopo Brussels, Ubelgiji na baadaye ataelekea Marekani na katika ziara hizo amesema ataelezea kile kilichomtokea Septemba 7, 2017, hali ya kisiasa nchini na mambo mengine.

Katika waraka wake huo alioutoa Januari 5, Lissu alitaja matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu huku pia akihoji sababu ya Bunge kutogharamia matibabu yake, mambo ambayo pia amesema kwamba atayaeleza katika ziara yake hiyo.

Waraka huo wenye kichwa cha habari ‘Mwaka mpya 2019, Mwaka wa kurudisha demokrasia, haki za binadamu na utu wetu Tanzania’ umegusia pia masuala ya haki za binadamu yakiwamo matukio ya utekaji, mauaji na mashambulio ya kudhuru mwili.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad