Tundu Lissu Ahofia Kuvuliwa Ubunge, Spika Ndugai Asema Hana Kibali cha Kuzurura Ulaya, Arudi Nyumbani


Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, (Chadema), amedai kuwa kuna mkakati wa kutaka kumvua Ubunge kwa madai kuwa ni mtoro bungeni.

Akizungumzia kwa undani mkakati wa kutaka kumvua Ubunge, kupitia waraka wake alioutoa, Lissu alidai kuwa kuna hoja inajengwa kuwa Mbunge huyo ni mtoro kwani hajaonekana Bungeni na hajamwandikia barua Katibu wa Bunge taarifa yoyote ya maandishi kuhusu kuumwa kwake wala matibabu yake.
 
Mbunge huyo ameeleza kuwa  hana sababu yoyote ya kutilia shaka taarifa hizi kwani waliomtonya ni watu wenye dhamana kubwa Bungeni na Serikalini ambao alidai hawaridhishwi na mkakati huo.

“Sijashangazwa na kuwepo kwa mkakati huu.Kilichonishangaza ni hoja zinazojengwa kuhalalisha uovu huu.

“Ni taarifa gani ya maandishi watu hawa wanahitaji wakati nilishambuliwa nikiwa kwenye vikao vya Bunge Dodoma?,” alihoji Lissu na kuongeza kuwa.

“Nilipelekwa Nairobi nikiwa sijitambui kutokea Hospitali Kuu ya Mkoa wa Dodoma, baada ya kikao kilichomshirikisha Katibu wa Bunge wakati huo, Dk. Thomas Kashilila, Spika Ndugai na Naibu Spika Dk. Tulia Ackson.

“Waziri wa Afya Ummy Mwalimu na Katibu Mkuu wake Dk. Ulisubisya Mpoki walikuwepo kwenye kikao hicho. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wakati huo, Mwigulu Nchemba, alikuwepo; na nilisindikizwa mpaka Nairobi Hospitali na daktari kutoka Hospitali Kuu ya Mkoa wa Dodoma, sasa taarifa gani inatafutwa,?” alihoji Lissu.

Kwa mujibu wa Lissu, wakati wote ambao amekuwa kwenye matibabu, uongozi wa Bunge umewasiliana kwa maandishi na mwakilishi wa familia yake kuhusu matibabu yake na wametoa matamko mengi hadharani kuhusu kushambuliwa kwake.

“Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amekuja kuniona nikiwa hospitalini Nairobi; Balozi wa Tanzania Ubelgiji, Joseph Sokoine, amekuja kuniona hospitalini Leuven mara mbili.

“Ni Spika Ndugai na uongozi wote wa Bunge, akiwemo Katibu wa Bunge, Steven Kagaigai, na maofisa wake, ndio hawajawahi kukanyaga hospitalini kuja kumwangalia mgonjwa wao, aliyeumizwa vibaya akiwa Bungeni,” amesema Mbunge huyo.

Alipoulizwa  kuhusu madai hayo, Spika Ndugai amesema hajui kama kuna mkakati wa kumvua Ubunge, lakini kwenye hoja ya utoro kweli Lissu ni mtoro.

“Kila mtu anajua Tundu Lissu ni mgonjwa na anapata matibabu Ubelgiji, sasa ukisikia ametoka Ubelgiji na kwenda sijui Uingereza na Spika hana taarifa na analipwa mshahara, huyo mtu ni mtoro, mwambieni arudi nyumbani kama ameshapona,” alisema Ndugai

Ndugai alisema Lissu anapaswa kutambua kuwa hana ruhusa ya kuzurura nje ya nchi.

“Yeye ametoka kuugua aache uzushi arudi nyumbani. Kitu muhimu ni kwamba ajue hana ruhusa ya Spika ya kuwa huko anakozurura.

"Wakati wenzake tuko bungeni tunafanya kazi za wananchi yeye yuko huko nje  kuipaka matope nchi yetu.” Alisema Ndugai
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad