Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 04 Januari, 2019 ameshuhudia utiaji saini wa mkataba wa mauziano ya mahindi kati ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Shirika la Chakula Duniani (WFP) uliofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Mkataba huo umetiwa saini na Kaimu Mtendaji Mkuu wa NFRA Bi. Vumilia Zikankuba na Mwakilishi na Mkurugenzi Mkazi wa WFP hapa nchini Bw. Michael Danford, ambapo WFP itanunua tani 36,000 zenye thamani ya shilingi Bilioni 21 kutoka NFRA.
Mahindi hayo ni sehemu ya tani 160,000 za chakula zenye thamani ya shilingi Bilioni 132.2 zilizonunuliwa na WFP nchini Tanzania katika mwaka 2018, ikiwa ni ongezeko la kutoka shilingi Bilioni 63.6 zilizotumika kununua chakula katika mwaka 2017.
"Ni wajibu wetu hizi fedha zote zinazokuja kusaidia wenzetu wakimbizi katika nchi nyingine wenye shida sisi tupate ‘reciprocal process’ ya kufaidika na matatizo yao. wao wapigane kule sisi tupate hela,” amesema Rais Magufuli.
“Sijasema kwamba wanapenda kupigana lakini kupigana kwao pia kuwe na faida kwetu, kwa sababu hata tusipowapa chakula bado watapigana tu, tunataka wasipigane lakini wakipigana sisi tuwe tumefaidika tukiwa na amani.”
“Nyinyi NFRA wapeni hawa WFP tani zote 45,000 wanazozihitaji, na hata wakihitaji tani 100,000 wapeni au hata 200,000 wapeni, mkipata hizo fedha nendeni mkanunue mazao ya wakulima wanaohangaika na soko. Lakini pia punguzeni matumizi makubwa ya fedha za kugharamia zoezi la ununuzi wa mazao” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Hafla ya utiaji saini mkataba huo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Omary Mgumba, Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe. Elias Kwandikwa, Makatibu Wakuu, viongozi wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama na wakuu wa taasisi mbalimbali.