Miamba ya soka ya ligi kuu Tanzania Bara Simba inatarajia kushuka uwanjani tarehe 11/1/2019 kutupa karata yake ya kwanza michuano ya Klabu bingwa barani Afrika dhidi ya JS Saoura FC kutoka Algeria mchezo wa kundi ‘D’ kuna timu za Al Ahly ya Misri na AS Vita Club ya DR Congo.
Kuelekea michezo hiyo ya kundi ‘D’ Bongo5 inakufanyia uchambuzi wa kila timu itakayo cheza na wawakilishi hao wa Tanzania Simba ambapo kwa leo tunaanza na klabu ya JS Saoura ya Algeria ambapo jina lake kamili inajulikana kama Jeunesse Sportive de laSaoura.
Klabu ya JS Saoura kutoka Algeria imekutana na timu mbili kabla ya kuingia hatua hii ya makundi kama ilivyo kwa Simba, ambapo mchezo wao wa awali waliwafunga SC Gagnoa kutoka nchini Ivory Coast kwa mabao 2 – 0 nyumbani na sare tasa ya 0 – 0 wakiwa ugenini.
Mchezo wao wa pili baada waliwafunga mabingwa wa ligi ya Morocco klabu ya IR Tanger mabao 2- 0 nyumbani na na kuchezea kichapo cha bao 1 – 0 ugenini na hivyo kupata kuingia hatua hiyo ya makundi kwa tofauti ya bao moja.
Hivyo mpaka wanapata nafasi ya kutinga hatua hiyo ya makundi JS Saoura wamefunga jumla ya mabao manne huku wakiruhusu nyavu zao kuguswa mara moja pekee.
JS Saoura FC yenye maskani yake Meridja siyo timu kongwe ukilinganisha na mpinzani wake Simba, yenyewe imeanzishwa mwaka 2008 huku moja kati ya uzi wao wa uwanjani ukiwa ni warangi ya Njano na Kijani.
Timu hii ambayo inatarajia kushuka dimbani Ijumaahii, kwa maana ya 4/1/2019 kuwakabili JS Kabylie wananolewa na kocha, Nabil Neghiz akiwa hana muda mrefu sana toka kukabidhiwa kibarua hicho mwezi machi mwaka jana 2018.
Kutokana na kuanzishwa kwake mwaka 2008 hivyo wana misimu saba pekee kwenye ligi kuu ya nchi hiyo maarufu kama League Professionelle 1, hasa ukizingatia walipanda daraja mwaka 2012 wakiwa hawana hata taji la Algeria na wakiwa wamewatimua kazi zaidi ya makocha 21 mpaka sasa.
Msimu wao mzuri ligi kuu kuliko wote toka kuanzishwa kwake ulikuwa wa mwaka 2015/16 na 2017/18 ambapo walifanikiwa kumaliza nafasi ya pili kwenye msimamo.
Hata hivyo wana historia nzuri kwenye uwanja wao wa nyumbani wakiwahi kucheza mechi 58 pasipo kupoteza kuanzia 6/2/15 mpaka 15/9/2018.
Upande wa wachezaji humtegemea zaidi mshambuliaji wao raia wa Algeria, Moustapha Djallit pamoja na Winga hatari, Sammar Zaid wakati langoni kukiwa na Nateche. Wengine ni Sid AliYahia-Cheriff, Sid Ahmed Aouedj, na Mohamed Boulaouidet. Hivi karibuni wamemuongeza Mtanzania Thomas Ulimwengu kwenye safu yake ya ushambuliaji .