Hatua hiyo ya wizara ya mambo ya ndani ya Marekani ambayo haikutangazwa, na ambayo haijawahi kuripotiwa, iliishusha hadhi ya kidiplomasia ya ujumbe wa Umoja wa Ulaya mjini Washington kutoka nchi mwanachama hadi shirika la kimataifa.
"Hatufahamu hasa lini walipochukua hatua hiyo, kwa sababu walisahau kutuarifu," afisa mmoja anayeifahamu vizuri kadhia hiyo ameiambia DW katika mahojiano maalumu.
Ninaweza kuthibitisha uamuzi huu haujapokelewa vyema mjini Brussels," akasema afisa huyo na kuongeza kwamba suala hilo na jibu rasmi la Umoja wa Ulaya bado vinajadiliwa.
Baada ya ujumbe wa Umoja wa Ulaya kutambua kwamba balozi wake mjini Washington hakualikwa kuhudhuria matukio muhimu mwishoni mwa mwaka uliopita, maafisa walioandaa mazishi ya rais wa zamani wa Marekani, George H.W Bush, walitoa thibitisho la mwisho kwa wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya kwamba hadhi ya uwakilishi ilikuwa imeshushwa.
Wanadiplomasia wanaamini hatua hiyo ilianza kutekelezwa mwishoni mwa mwezi wa Oktoba au mapema Novemba.
Afisa wa Umoja wa Ulaya amesema, katika tukio hilo la Desemba 5, wakati wanadiplomasia walipokuwa wakikusanyika mjini Washington kutoa heshima zao, balozi wa Umoja wa Ulaya mjini Washington, David O'Sullivan, hakuitwa katika hali ya kawaida ya kufuata orodha ya mabalozi kuanzia waliohudumu kwa muda mrefu hadi wale waliohudumu kwa kipindi kifupi. Badala yake aliitwa kama mtu wa mwisho kabisa katika orodha hiyo.
Kabla ya kushushwa hadhi, O'Sullivan, ambaye amehudumu kama balozi wa Umoja wa Ulaya mjini Washington tangu mwaka 2014, angekuwa miongoni mwa mabalozi 20 au 30 kati ya wajumbe zaidi ya 150 wa kigeni wanaohudumu katika mji mkuu huo wa Marekani.