Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es salaam Lazaro Mambosasa, amesema hana taarifa yoyote ya kukamatwa kwa gari ya Mbunge wa Jimbo la Kibiti, kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM, Ally Ungando ambaye taarifa za kukamatwa kwa gari yake zilianza kusambaa leo kupitia mitandao.
Kauli hiyo ya Mambosasa ameitoa leo wakati akizungumza na www.eatv.tv ilipotaka kuthibitisha juu ya taarifa ya kushikiliwa kwa gari ya mbunge huyo ambaye ilisadikika ilikamatwa kwa kosa la kusafirisha mbao kinyume na taratibu za usafirishaji za malighafi za misitu nchini.
"Hizo taarifa za kukamatwa kwa gari ya Mbunge mimi sina taarifa labda amekamatwa na wengine ila mimi sina taarifa", - Mambosasa.
Akizungumza na baadhi ya vyombo vya habari nchini, Mbunge wa Jimbo Kibiti Abdallah Ungando, alithibitisha kukamatwa kwa gari lake na jeshi la polisi kwa tuhuma za kusafirisha mbao kinyume na taratibu ambapo lilikamatwa wiki hii lilipokuwa likitokea Kibiti likielekea Jijini Dar es salaam ambapo likiwa limebeba shehena hiyo ya mizigo.
Mbunge Ungando amesema "mimi ni mbunge wa CCM na nimeombwa gari na CCM sasa ungekuwa wewe ungefanyaje ? nikaona nisaidie chama changu lakini sikujua yote hayo na kama ningetaka kusafirisha mbao basi ningetumia malori yangu" amesema Ungando.