Wafanyakazi wawili wa kampuni ya simu ya Airtel na wengine tisa wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka saba yakiwemo ya kuingilia mifumo ya mawasiliano ya kampuni hiyo.
Akiwasomea mashtaka, Wakili wa Serikali, Ester Martin akisaidiana na Erick Shija, alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Kelvin Mhina kuwa kati ya Septemba 9 na Desemba 24 mwaka jana, jijini Dar es Salaam washtakiwa walikula njama ya kutenda kosa la wizi.
Katika shtaka la pili alidai siku na mahali hapo, washtakiwa hao huku wakijua kuwa ni kinyume cha sheria walijaribu kutenda kosa la wizi.
Katika shtaka la tatu, washtakiwa Laizer na Mwenda kwa makusudi na kinyume cha sheria walisababisha kuingilia mfumo wa mawasiliano wa kampuni ya Airtel bila ya kuwa na kibali.
Shtaka la nne alidai kuwa washtakiwa wote walitoa taarifa za mfumo wa mawasiliano wa kampuni hiyo kinyume cha sheria.
Waliofikishwa mahakamani ni Rodgers Laizer na Nancy Mwenda ambao ni wafanyakazi wa Airtel, Erick Fidelisi, Zephaniah Maduhu, Anthony Masaki, Lumuli Stanford, Ndeshiwonasiya Malle, Davis Waseda, Goodluck Nyakira, Michael Onyango na Sylvester Onyango.
Washtakiwa walikana kutenda makosa hayo na mshtakiwa Masaki, Stanford, Eased na Mwenda walipata dhamana na wengine wamepelekwa rumande kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana. Kesi ime iatatajwa Januari 29, mwaka huu kwa kuwa upelelezi haujakamilika.
Wafanyakazi Wawili Airtel na Wengine 9 Kortini Kwa Kuingilia Mifumo ya Mawasiliano ya Kampuni Hiyo
0
January 17, 2019
Tags