KAMATI ya Rufaa ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) inatarajia kutoa hukumu ya rufaa ya wagombea wawili wa Klabu ya Yanga waliopinga kuenguliwa katika usaili uliofanyika mwaka jana ikiwa ni pamoja na kubandika majina ya wagombea watakaotakiwa kupiga kampeni.
Wagombea wa Yanga ambao walikata rufaa katika Kamati ya Rufaa ya TFF ni Yona Kevela ambaye alichukua fomu ya kugombea nafasi mbili tofauti ya uenyekiti na makamu pamoja na Leonard Marango aliyekuwa akiwania nafasi ya ujumbe.
Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliwaengua wagombea hao kutokana na kutotimiza vigezo katika kipindi cha usaili, hivyo kamati ya rufaa inatarajia kutoa hukumu leo Ijumaa baada ya kukutana na kupitia malalamiko yao na kubandika majina.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Malangwe Mchungahela alisema: “Kamati ya Rufaa itatoa maamuzi kesho (leo) juu ya wagombea waliokata rufaa na kubandika majina ya wagombea watakaofanya kampeni ili taratibu nyingine ziweze kuendelea.” Yanga inatarajia kufanya uchaguzi wake mkuu Januari 13 ambapo kampeni zinatarajia kuanza siku tano kabla ya uchaguzi huo kufanyika.