Waitara Amsimamisha Kazi Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa,

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara, ameagiza kumsimamisha kazi Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, ili kupisha uchunguzi wa fedha zilizotumika katika ujenzi wa mabweni mawili ya wasichana katika Shule ya Sekondari Isimila.

Waitara alichukua uamuzi huo jana akiwa mkoani Iringa, baada ya kukagua ujenzi wa mabweni hayo yaliyojengwa chini ya kiwango kulinganisha na fedha zilizotumika. Ujenzi huo umegharimu Sh. milioni 184 huku majengo yakiwa hayajamalizika yakiwa yanahitaji fedha zingine ili kukamilika.

Kutokana na hali hiyo, Waitara alionyesha kukerwa na ujenzi huo ambao umetumia fedha za serikali na nguvu za wananchi na umesimama kutokana na kutokamilika.

Alimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Robert Masunya, kumsimamisha kazi mhandisi huyo, Nestory Chacha, mpaka uchunguzi utakapofanyika ili hatua za kinidhamu zichukuliwe.

‘’Naona ninyi mnaichezea serikali, haiwezekani serikali itoe fedha kujenga mabweni ili watoto wetu waepukane na vitendo vya kikatili vikiwamo ubakaji na mimba za utotoni wasome katika mazingira mazuri na hatimaye kufikia ndoto zao. Sasa leo (jana) ninaagiza mhandisi apewe adhabu kali na ifikapo Februari 5, taarifa ya uchunguzi iwe imeshanifikia,’’ alisema.

Aidha, aliwataka wakuu wa wilaya mkoani hapa kuhakikisha wanasimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa na fedha za serikali ili kukamilika kwa wakati huku ikiwa na kiwango kinachostahili.

Pia alionyeshwa kusikitisha na taarifa ya shule hiyo kuhusu wanafunzi 43 ambao wameshindwa kuanza kidato cha kwanza mwaka huu kutokana na utoro.

Waitara alisema pamoja na serikali kuipa kipaumbele sekta ya elimu, kumekuwa na utoro wa wananfunzi waliochanguliwa kuanza masomo. Aliutaka uongozi wa shule na wilaya kufuatilia kwa makini ili wale waliochaguliwa waanze masomo mara moja.

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad