Kiungo Haruna Niyonzima wa Simba, ametolea ufafanuzi suala la wachezaji wa klabu hiyo kutoroka kambini usiku wa kuamkia mchezo wao wa nusu fainali ya SportPesa Cup dhidi ya Bandari FC ambapo ilifungwa mabao 2-1.
Niyonzima amesema suala hilo linakuzwa tu na watu lakini wachezaji wao wanafanya mambo ambayo wanajua sio hatari kwa mchezo wa soka.
''Wachezaji hawakutoroka na hakuna ushahidi wa hilo, wachezaji walifanya yote yanayowahusu ikiwemo kujilinda lakini tumejifunza kutokana na makosa na tunaelekea kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika'', amesema.
Kuhusu video ya mlinzi wa Simba Pascal Wawa ambayo ilisambaa mtandaoni ikimwonesha akiwa kwenye 'party', Niyonzima amesema haikuwa siku hiyo ila watu wameunganisha tu matukio.
Simba imeondoka leo nchini kuelekea Misri kwaajili ya mchezo wake wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly utakaopigwa Februari 2.