Watupwa Mahabusu kwa Kumdanganya Naibu Waziri


Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Juma Aweso ameamuru kukamatwa na kuwekwa mahabusu kwa Mhandisi wa Maji wa wilaya ya Monduli, Charles Saidea na Mkandarasi kutoka kampuni ya Meru Constructions, Ayo Jeremia kwa tuhuma za kufanya udanganyifu katika miradi wa maji inayoendelea.


Askari Polisi akiwa amewashikilia ,Mhandisi wa Maji wa wilaya ya Monduli,Charles Saidea (kulia) na Mkandarasi, Ayo Jeremia wa kampuni ya Meru Constructions mara baada ya Naibu Waziri kuamuru wakamatwe.

Waziri Aweso ametoa agizo hilo katika kijiji cha Lendinyika wakati wa ziara yake ya siku moja katika wilaya ya Monduli kukagua utekelezaji wa Miradi ya Maji katika vijiji 10 vya Halmashauri hiyo, ziara  ambayo hata hivyo alilazimika kuikatisha mara baada ya kubaini kuwepo kwa taarifa zinazokinzana na taarifa ya utekelezaji wa mradi wa maji wenye thamani ya Sh Bil 1 na Mil 79 .

Mbali na uwepo wa dosari nyingi za kiufundi ,mradi huo unaotajwa kukamilika kwa asilimia 85 bado haujaanza kutoa maji huku Mkandarasi akieleza kuidai Serikali sehemu ya fedha za mradi huo, jambo ambalo Mhandisi alionekana kupinga uwepo wa madai hayo.

Hoja ya kuwepo kwa Mabomba ya plastiki yaliyopita katika Makorongo iliibuliwa na mmoja wa wakazi wa kijiji cha Lendikinya Lemta Naisikie baada ya kutaka kujua kama ni sahihi kwa mkandarasi kupitisha Bomba hizo katika sehemu za wazi badala ya bomba za chuma.

“Swali langu ni moja, bomba zilizotandazwa kuleta maji katika kisima kuu,kuna sehemu za Makorongo zote zimewekwa hii bomba la mpira, hii naona ni changamoto afadhali ingewekwa bomba la chuma na maeneo mengine kuna mawe tungeomba mkandarasi atandaze bomba la chuma ili zisilete athari baadae” amesema Naisikie.

Baada ya kutolewa kwa hoja hiyo Naibu Waziri, Aweso aliamua kutembelea baadhi ya Makorongo na kujionea Bomba la Plastiki likiwa limepita juu badala ya Bomba la Chuma ndipo akaamua kutoa maelekezo.

“Viongozi wenu wote wanazungumzia swala la maji, Lendikinya ni moja ya vijiji vyenye changamoto kubwa sana ya maji, Mbunge wenu amepiga sana kelele kuhusu maji kwa wananchi wa Monduli, sasa sisi leo tumekuja hapa tumeona kuna mradi wa zaidi ya sh Bil 1 na Mil 79 lakini mradi uko zaidi ya asilimia 80 lakini maji kwa wananchi hakuna.” amesema Aweso

“Unawauliza wataalamu wetu wakupe taarifa zile sahihi, hawakupi, leo mwananchi huyu wa kawaida kabisa anakupa taarifa sahihi mahala ambapo yalitakiwa kuwekwa mabomba ya chuma yameweka mabomba ya plastiki na hakuna usimamizi wa aina yoyote.”  ameongeza Aweso.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad