YANGA ambayo kikosi chake chote kiko fiti inashusha mziki wote leo Alhamisi usiku kwenye Uwanja wa Taifa dhidi ya Biashara ambayo imeingia na mkwara mzito.
Ukiachana na ligi, hiyo ndiyo michuano pekee inayoweza kuwapa tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani.
Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera amesisitiza kutumia mbinu alizotumia Kocha wa Azam, Hans Van Pluijm dhidi ya Biashara ambazo zilimsaidia kupata ushindi wa 2-1.
“Niliwaona walivyocheza dhidi ya Azam, wameonyesha mabadiliko makubwa sana kwenye raundi hii ya pili.
“Sisi tumejitayarisha kukabiliana nao kwa sababu tumeona uwezo wao nafi kiri wachezaji pia wameona kuwa Biashara hawa ni tofauti na wale tuliowafunga kwenye ligi,” alisema Zahera ambaye anaishi karibu na ufukwe wa Bahari ya Hindi eneo la Kawe.
Lakini Kocha wa Biashara, ambaye pia mwanachama hai wa Simba, Amri Saidi amesisitiza kwa vyovyote itakavyokuwa lazima watawafunga Yanga. “Sisi tumejiandaa kushinda kwa hali yoyote ile, vijana wangu wana ari kubwa sana ya kupambana kwa bahati mzuri sina majeruhi hadi hivi sasa kwenye kikosi changu, wajipange,” alisema Said ambaye ni beki wa zamani wa Simba.