Klabu ya soka ya Yanga imetupwa nje ya michuano ya Mapinduzi Cup baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-1 kwenye mchezo uliomalizika usiku huu kwenye uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar.
Yanga imeaga michuano hiyo ikiwa na alama 3 ambazo ilizipata kwenye mchezo wake dhidi ya KVZ iliposhinda bao 1-0. Mchezo wa pili ilipoteza kwa mabao 3-0 kutoka wa Azam FC ambao ni mabingwa watetezi.
Kocha mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera hakuwa anaitupia jicho sana michuano hii na mara nyingi amekuwa akisisitiza kuwa haipo kwenye mipango yake kwani haiwezi kumpeleka popote kama ambavyo ligi kuu na kombe la shirikisho vinaweza kumpa nafasi ya kuwakilisha nchi kimataifa.
Zahera pia aliamua kupeleka kikosi cha pili huku wachezaji nyota akiwaacha Dar es salaam kwaajili ya programu maalumu ya kujiweka sawa kwenye ligi kuu soka Tanzania bara.
Yanga sasa imesaliwa na mchezo mmoja kwenye Kundi B lenye timu za KVZ, Malindi, Jamhuri na Azam FC. Kabla ya kurejea Dar es salaam Yanga itacheza na Jamhuri.