Unapoingia kwenye biashara kichwa kichwa bila kujua mambo yatakayokusaidia kukuweza kukua katika biashara hiyo elewa kuwa kama hautokuwa makini ipo siku biashara hiyo itakufa tu, na ukweli usipungua wafanyabiashara wengi, wao ndio huchangia kwa kiasi kikubwa biashara zao kufa.
Na zifutazo ndizo sababu za biashara nyingi kufa, hivyo mfanyabiashara ni lazima awe makini na mambo haya ili biashara yake isiweze kufa:
Kutokuwa na elimu ya biashara.
Ili kufanikiwa kibiashara ni lazima wewe kuwa na elimu ya kutosha kibiashara. Pengine unataka kujiuliza nitaipata wapi sasa? Sikiliza huhitaji gharama kubwa sana kuipata. Unaweza kujifunza kupitia semina, huwezi hilo unaweza kujifunza kupitia mitandao ya kuhamasisha au ukanunua vitabu vinavyohusu biashara ukajifunza polepole. Lakini kikubwa usiikose elimu hii, vinginevyo utapoteza mengi ikiwa pamoja na biashara yako.
Kuwa makini na matumizi ya pesa
Hakikisha matumizi yako yanakuwa ya gharama ya chini . ukitumia pesa vibaya Kama kwenye biashara yako huwezi kufika mbali. Ni lazima uwe na mpangilio mzuri wa matumizi yako ya pesa ili kuifanya biashara yako ikazidi kuendelea.Kuwa makini na pesa zako. Tofauti na hapo biashara yako itakufa tu hata kama sio leo, lakini lazima itakufa.
Kukosa ubunifu.
Ili uweze kukabiliana na ushindani, ubunifu ni muhimu sana katika biashara yako. Bila kuwa mbunifu huwezi kufanikiwa katika hiyo biashara kutokana na mazingira ya ushindani mkubwa tulionao kwa sasa. Kwa hiyo ni lazima kuwa mbunifu na kuifanya biashara yako ikaonekana ya tofauti na kukupa wateja wa kutosha.
Wengi wanaoshindwa kwenye biashara ni wale walioingia kwa kiburi cha mtaji mkubwa na kusahau ubunifu. Haijalishi unafanya biashara ndogo au kubwa weka ubunifu. Kila wakati tafuta ni kitu gani biashara yako inakosa, kisha kiboreshe zaidi. Jitahidi sana kuweka ubunifu ili kuifanya biashara yako iwe hai siku zote, vinginevyo utaiua.
Kukosa nidhamu.
Kama unaendesha biashara yako na ukakosa nidhamu ya kuiendesha biashara hiyo, elewa kabisa utakuwa na mchango mkubwa sana wa kuiua. Nidhamu ni msingi mkubwa sana wa mafanikio yoyote na sio biashara tu peke yake. Jaribu kuangalia watu wote wenye nidhamu ya kazi mafanikio yao yakoje? Bila shaka ni makubwa.
Biashara nyingi sana zinazokufa huku zikiwa na mtaji mkubwa mara nyingi hukosa nidhamu. Tuchukulie una duka la reja reja, huwezi kufanikiwa ikiwa unafungua na kufunga unavyotaka. Ni lazima uwe una nidhamu ya muda, nidhamu ya kuwajali wateja au nidhamu ya kauli nzuri. Kwa kukosa nidhamu hizi biashara itakufa tu hata iwe kubwa vipi.
Kukosa wateja.
Kati ya kiungo muhimu sana kwenye biashara yako ni wateja. Bila wateja hakuna biashara inayoweza kufanyika. Sasa kama utakuwa huna wateja hiyo inamaanisha biashara yako kwa vyovyote vile itaenda kufa hata ufanye nini. Maana hao ndio wawezeshaji wakubwa kwenye biashara yako kuendelea.
Sasa huwa zipo sababu zinazopelekea biashara hii ikakosa wateja na nyingine ikawa na watej wengi. Hivyo ni vyema ukazijua sababu hizo ili zikusaidie kuweza kujenga biashara ya uhakika na yenye mafanikio makubwa.
Kukosa vipaumbele.
Biashara yoyote iwe inanza au inaendelea ni lazima iwe na vipaumbele vya msingi ambavyo vinatakiwa vifuatwe kila siku. Kama kipaumbele chako kimojawapo ni kutaka kukuza mtaji ni vyema ukawa makini kuhakikisha hilo linatimia na kutekelezeka kwa haraka sana.
Lakini kama pia vipaumbele vyako ni kuhakikisha unadumisha mahusianao mazuri na wateja wako, pia ni bora ukatekeleza. Unapokosa vipaumbele hata vile unavyoviona ni vidogo ni rahisi sana kwa biashara yako kuweza kufa na kushindwa kuendelea hata kama ina mtaji wa kutosha. Kwa sababu hapa tunasema biashara inakuwa inakosa dira maalumu.