Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya spika Ndugai kumtaka Profesa Assad kwenda mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kinga, Maadili na Madaraka ya Bunge Januari 21, kwa kitendo cha kuliita Bunge kuwa ni dhaifu wakati akihojiwa na Radio ya Umoja wa Mataifa nchini Marekani hivi karibuni, ambapo amesema akishindwa kufika mwenyewe atafuatwa na pingu.
Katika barua hiyo, Zitto pia ametuma nakala kwa maspika wa mabunge yote ya Afrika kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola na Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC), na Wadhibiti na Wakaguzi Wakuu wa Hesabu za Serikali wote wa Jumuiya ya Madola, kuwataka kuzungumza na Spika Ndugai kuachana na kitendo hatari cha kudidimiza misingi ya uwajibikaji nchini.
“Kwa kuwa Bunge la Tanzania ni mwanachama wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA), naomba uingilie kati kutatua kidiplomasia kwa kuzungumza na Spika wa Bunge la Tanzania, ukimueleza hatari za uamuzi wake.
“Naamini kuwa suala hilo linaweza kutatuliwa kwa urahisi na kuboresha uhusiano kati ya taasisi hizo mbili muhimu yaani Bunge na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, ambayo hutegemeana,” imesema sehemu ya barua hiyo ya Zitto.