28 Watiwa Mbaroni Mauaji ya Watoto Njombe

28 Watiwa Mbaroni Mauaji ya Watoto Njombe
Baadhi ya waganga wa jadi wasiokuwa na nia Njema wameanza kutoroka mkoani Njombe na kukimbilia mikoa ya jirani kutokana na msako mkali wa jeshi la polisi unaoendelea mkoani humo ili kuwabaini wanaojihusisha na ramli chonganishi zinazosababisha mauaji ya watoto.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake,kamanda wa polisi mkoa wa Njombe RENATHA MZINGA amesema kuwa jeshi la polisi halitaweza kuwaacha wale wote waliokuwa na nia ovu na kuwatafuta popote pale walipo.

“Tunao waganga 6 tunaowashikilia mpaka sasa kwa mahojiano na tulivyoanza na kamata kamata wale ambao wana nia ovu wanaendelea kukimbia lakini hata hivyo  tunaendelea kuwafuatilia kule waliko hatutawaacha  kwasababu tunaamini kabisa wao ndio waliotoa maelekezo ambayo yanaangamiza kizazi chetu hiki cha watoto wadogo”alisema kamanda Mzinga

Aidha kamanda huyo wa polisi amesema kuwa mpaka sasa jeshi hilo la polisi limekwisha hakiki leseni karibu 50 za waganga wa jadi huku wakiendelea na zoezi hilo.

“Kwa kweli tunaendelea vizuri na tumekwisha hakiki waganga karibia 50 lakini tunaendelea kushirikiana na chama cha waganga mkoa wa Njombe katika zoezi hilo pamoja na mratibu wa waganga wa tiba asili na tiba mbadala mkoa na tunahakikisha waganga wanaobaki mkoa wa Njombe ni wale wanaofanya kazi za halali”alisema kamanda

Katika hatua nyingine jeshi hilo la polisi limesema kuwa mpaka sasa linataarifa ya mtoto mmoja tu aliyepotea mwenye umri wa miaka 7 kutoka kijiji cha Ikando ambaye bado hajapatikana.

“Mpaka sasa hivi ni mtoto mmoja tu ambaye amepotea hatujamuona ambaye ana miaka 7 kule kijiji cha ikando lakini wengine wote ni hawa waliouawa”aliongeza kamanda

Jumla ya watu 28 wakiwemo waganga wa jadi,wafanyabiashara pamoja na wananchi waliojichukulia sheria mkononi na kufanya mauaji dhidi ya vijana wanaohisiwa kutekeleza mauji ya watoto wanashikiliwa na polisi kwa ajili ya upelelezi huku mpaka sasa jumla ya watoto 7 wamepoteza maisha kwa matukio ya mauaji mkoani Njombe.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad