Mbunge wa Jimbo la Siha, Godwin Mollel amesema yuko tayari kushtakiwa kufuatia madai aliyoyatoa dhidi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA juu suala la shambulio la Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu .
Akiwa Bungeni mapema wili iliyopita Mbunge huyo alihusisha madai ya kushambuliwa kwa mbunge huyo wa Singida Mashariki na kueleza kuwa hatua hiyo ililenga kuichafua serikali na yuko tayari kutoa ushahidi mahakamani.
Akizungumza na www.eatv.tv Dkt Mollel amesema, "kuhusu mimi kushtakiwa sina shida na niliwaambia CHADEMA wanishtaki tena ili nikasaidie ila wakitaka wanipe platfom ili nikazungumzie zaidi suala hili."
"Suala lingine ni kwamba nikipata fursa ya kusema nitahoji vingi kwa sababu CHADEMA wanapokea hela kutoka nje ya nchi kwa hiyo nitaomba wanieleze wanapeleka wapi hizo fedha", ameongeza Mollel.
Godwin Mollel ni miongoni mwa wabunge ambao walikuwa upinzani lakini baadaye walitangaza kuachia nafasi zao na kuhamia CCM kwa kile walichokidai kuwa ni kuunga mkono jitihada za Rais Dkt John Pombe Magufuli.