Mchezaji Chris Casper ambaye anaweza kuwa ndio mchezaji aliyewahi kupita Manchester United na kustaafu soka katika umri mdogo zaidi, amesema mafanikio ya Alex Ferguson kwenye 'Class of '92' yalisababishwa na kocha Eric Harrison.
Chris Casper ameyasema hayo kufuatia kifo cha kocha huyo aliyewafundisha nyota mbalimbali katika timu ya vijana ya Manchester United ambao walikuja kuwa na mafanikio makubwa kwenye timu ya wakubwa chini ya Ferguson.
Eric Harrison amefariki Februari 13, 2019 huko Mytholmroyd, Burnley, Uingereza akiwa na miaka 81, ambapo nyota mbalimbali wa Manchester United wameonesha kuguswa na msiba huo.
"Wakati huo Eric ndio alikuwa mtu wa kwanza kufanya kazi na wewe ukiingia ndani ya timu na tulikuwa na umri wa chini ya miaka 16 kwahiyo wengi tulikuwa 14 na 15 na aliweka misingi juu yetu akisisitiza zaidi nidhamu na kujituma jambo ambalo lilirahisisha sana kazi kwa Ferguson kwasababu alipata watu waliokuwa kamili'', amesema Chris Casper ambaye alistaafu akiwa na miaka 24 kutokana na kuandamwa na majeruhi.
Chris Casper anaamini hata mafanikio ya Ryan Giggs, Paul Scholes, David Beckham na wachezaji wengine wa timu ya vijana ya Man United wakati huo yaliletwa na Eric Harrison na sio Ferguson kama wengi wanavyodhani.
Giggs, Scholes, Gary Neville, Chris Casper, Beckham na Butt ni miongoni mwa wachezaji wa Manchester United waliopata nafasi timu ya wakubwa kwa pamoja msimu wa 1991/92.