Barrick Gold Yaahidi Mambo Mazito Kwa Rais Magufuli, Mabilioni ya Shilingi Kulipwa Mwezi Ujao



Rais John Magufuli jana alikutana na kufanya mazungumzo na Ofisa Mwendeshaji Mkuu wa Kampuni ya Barrick Gold anayeshughulikia Afrika na Mashariki ya Kati, Dk. Willem Jacobs, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu ilisema katika mazungumzo hayo, Dk. Jacobs alimhakikishia Rais kuwa watalipa fedha walizoahidi mwezi ujao.

Baada ya mazungumzo hayo, kwa mujibu wa taarifa hiyo, Dk. Jacobs aliyeongozana na washauri wa Barrick Gold Corporation, Rich Haddock, Duncan Bullivant na Wicus du Preez, alisema wamekutana na Rais Magufuli ili kumhakikishia kuwa makubaliano yaliyofikiwa Oktoba 19, 2017 watayatekeleza kikamilifu baada ya kampuni kubwa ya uchimbaji dhahabu ya Rand Gold ya Afrika Kusini kuungana na Barrick Gold Corporation katika umiliki, uwekezaji na menejimenti.

Dk. Jacobs alisema hakuna kitakachokuwa tofauti na makubaliano yaliyofikiwa awali ambayo yaliongozwa na Mwenyekiti Mtendaji wa Barrick Gold Corporation, Prof. John Thornton, ikiwemo Barrick Gold Corporation kuilipa serikali ya Tanzania kifuta machozi cha Dola za Marekani Milioni 300 (sawa na Sh. Bilioni 682.5).

Makubaliano mengine ni kuendelea na uwekezaji kwa ubia kati ya serikali ya Tanzania na Barrick Gold na mgawanyo wa mapato ya kiuchumi kwa uwiano wa asilimia 50 kwa 50 kati ya Tanzania na kampuni hiyo.

Taarifa hiyo ilisema Dk. Jacobs alimpongeza Rais Magufuli kwa jitihada zake za kusimamia maslahi ya Watanzania katika rasilimali za nchi na kwamba pamoja na ukweli kwamba Rais yuko katika njia sahihi, akiwa Mwafrika anaunga mkono juhudi hizo kwa kuwa ndio mwelekeo sahihi ambao nchi za Afrika zinapaswa kuufuata.

“Mimi ni Mwafrika na sisi sote ni Waafrika. Anachokifanya Rais Magufuli ni sahihi kabisa, anahakikisha utajiri wa rasilimali uliopo unabainishwa na unawanufaisha Watanzania ndiyo maana tupo hapa kwa sababu tunakubaliana na Rais,” alisema kama alivyokaririwa na taarifa hiyo.

“Na hivi ndivyo sisi Waafrika tunapaswa kufanya kwa rasilimali zetu, na sisi tunahakikisha tunafanya kazi vizuri na serikali na jamii kulinda rasilimali hizi, kumbuka rasilimali hizi ni za wananchi, jukumu langu kama mwekezaji ni kubadili hayo madini kuwa kodi na ajira kwa Tanzania na pia kampuni yangu kupata faida yake halali,” aliongeza.

Alibainisha kuwa baada ya muungano huo wa Rand Gold na Barrick Gold, sasa kampuni mpya ya Barrick Gold imekuwa kubwa inayoongoza kwa umiliki wa rasilimali za dhahabu duniani ikimiliki rasilimali tano kati ya 10 na kwamba kutokana na uwezo huo, Barrick Gold Corporation sasa imejiimarisha zaidi kiuwekezaji na utaalamu na iko tayari kushirikiana na Tanzania kuhakikisha dhahabu iliyopo inaleta manufaa kwa pande zote mbili yaani Watanzania na mwekezaji.

Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi, ambaye aliongoza timu ya majadiliano kwa niaba ya serikali ya Tanzania na Barrick Gold, alisema nyaraka za makubaliano hayo zimekamilika na kwamba kinachosubiriwa ni utekelezaji wa unaotarajiwa kukamilika ifikapo mwisho wa Machi, mwaka huu.

“Baada ya muungano wao (Rand Gold na Barrick Gold Corporation) hii sasa ni timu mpya na tumewaona ni watu ambao sasa wako tayari kutekeleza yale yote yaliyokubaliwa. Sasa ni kwa kila upande kwenda kwenye vyombo vyake vinavyohusika kufanya uamuzi wa mwisho ili utekelezaji ufanyike,” alisema Kabudi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad