Beki wa Harambee Stars ya Kenya, atuhumiwa kupokea mamilioni ya fedha ili kuruhusu timu yake ya taifa kufungwa
0
February 05, 2019
Shirikisho la soka duniani (FIFA) limeanza uchunguzi dhidi ya beki wa Harambee Stars, George Owino Audi kufuatia kusema kuwa amelipwa mamilioni ya fedha ili kuihujumu timu yake ya taifa ya Kenya kwenye michezo kadhaa ya kimataifa.
Kwenye ripoti ya kwanza ya uchunguzi yenye kurasa 10, FIFA imeanzisha kesi dhidi ya beki huyo, George Owino Audi kutokana na kukiuka maadili hayo ya soka kati ya June 2009 na 2011.
Kwa mujibu wa upangaji wa mechi kwenye ripoti ya FIFA, George Owino Audi ambaye ni beki wa Harambee Stars amepokea kiasi cha milioni tatu hadi sita ili kuhakikisha timu yake inapoteza.
Kwa mujibu wa chombo cha habari cha Daily Nation, FIFA imetoa ripoti ya Mwezi Septemba mwaka 2018 kuwa wamegundua Owino alikuwa akifanya mawasiliano kupitia email 177 walizozipata ambazo zikionyesha kupanga matokeo ya mechi za Harambee Stars kwa kushirikiana na Wilson Raj Perumal mtu ambaye anatambulika kama ameshindikana, kwenye tabia za kupanga matokeo ya michezo mbalimbali duniani na kuwahi hata kushtakiwa na kuwekwa kifungoni.
Taarifa za FIFA zimefika mbali zaidi na kudai kuwa nyota huyo mwenye umri wa miaka 37 amekiri kufanya hivyo huku akiwahamasisha baadhi ya wachezaji wenzake kuihujumu timu yao ya taifa na kupokea fedha kutoka kwa Perumal.
“Nina ofa kwaajili yako ya kucheza Australia,unachotakiwa ni kuwa kimya , ligi inatarajia kuanza Agosti na nitakusajili Mwezi Juni 2010, kuwa mbali na klabu nyingine” ameandika, Perumal ikiwa ni ombi kwenda kwa Owino, Machi 25, 2010.
“Unahitaji kucheza ndani ya klabu yangu ?, inatakiwa kuwa siri,” iliandikwa na Perumal siku iliyofuata Machi 26, 2010.
Ambapo Owino alijibu “Ndio moja kati ya uliyosema ni Australia natumaini ni kuzuri zaidi kibiashara.”
Perumal ambaye hapo kabla aliwahi kufungwa huko Finland na Hungary kufuatia tuhuma kama hizo za upangaji matokeo alimuandikia email, Owino ikimtaka kuihujumu klabu yake mpya ya Australia mara baada ya kujiunga.
“Dhumuni la kukupeleka pale ni inshu za kibiashara, hivyo unatakiwa kuwa muaminifu kwangu. Utakuwa unapokea mshahara wa dola 30,000 kila mwezi kama nitasema mfungwe lazima ufanye nitakachokuambia nje ya hapo kamwe huwezi kuuona mshahara wako.”
Owino kisha akajibu email hiyo Machi 29, 2010 akikubaliana na Perumal na hata kukubali kufungwa kwenye mchezo wake wa kwanza mara baada ya kujiunga na klabu hiyo.
“Sawa hakuna tatizo kwasababu hata mimi nahitaji maisha mazuri kwaajili yangu na familia hivyo nitafanya kama utakavyoniambia.” Kisha baada ya hapo akaulizia safari yake ya Australia.
“Tutasaini mkataba mwishoni mwa mwezi, na tunatarajia kuwasili wiki ya pili ya mwezi Mei,” alijibu Perumal.
“Lazima uamke, unahitaji fedha au matokeo, kama utamaliza kwa kupoteza 1 – 0 dhidi ya Tunisia haita utakuwa hujafanya kitu. Ninahitaji ufungwe 3 – 0 hata 2 – 0 ni matokeo ya kawaida.” Perumal alimuonya Owino.
“Nahitaji upambane ndani ya dakika 25 ufungwe bao 1, kisha kati ya dakika 30 – 45 ufungwe la pili na la tatu kati ya dakika 65 na 80.”
Kwenye email hiyo, iliwataja wachezaji wawili wa timu ya taifa ya Kenya ambao ni Julius na Pascal.
Mwaka 2010 michuano ya kombe la dunia, Kenya ikicheza dhidi ya Tunisia
hatua ya kufuzu fainali hizo mchezo ukichezwa Octoba 11, 2009 inadaiwa kuwa miongoni mwa mechi zilizohujumiwa.
Tags