BUNDA: Wanafunzi 103 Washindwa Kujiunga Sekondari

JUMLA ya wanafunzi 103 waliomaliza elimu ya msingi mwaka jana na kuchaguliwa kujiunga na  sekondari ya kata ya Hunyari iliyoko katika wilaya ya Bunda mkoani Mara, bado hawajajiunga katika shule hiyo kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa.

Taarifa hiyo imetolewa na mkuu wa shule hiyo Desdery Fabian, kwenye mwendelezo wa sehemu ya sherehe za miaka 42 ya kuzaliwa kwa CCM, zilizofanyika katika viwanja vya shule hiyo iliyoko katika tarafa ya Chamriho wilayani hapa.

Fabiani amesema kuwa wanafunzi wa kidato cha kwanza waliochaguliwa mwaka huu kujiunga na sekondari katika shule hiyo ni 253, lakini waliokwishapata nafasi kulingana na vyumba vya madarasa vilivypo ni 150 na kubaki wanafunzi 103.

Aidha, amesema kuwa changamoto nyingine inayoikabili shule hiyo ni pamoja na utoro warejareja na sugu kwa wanafunzi, na kwamba utoro huo unawahusisha wazazi kwani hawashirikiani na walimu ipasavyo, kuhakikisha watoto wao wanahudhuria shule bila kukosa.

Ameongeza kuwa  changamoto nyingine ni kuongezeka kwa watoto wa kike kupata ujauzito na kwamba tatizo hilo ni kubwa, ambapo inadaiwa kuwa linafadhiliwa na wazazi wenyewe.

Amesema kuwa uongozi wa shule unajitahidi kudhibiti tatizo hilo, lakini unaelemewa kutokana na mazingira yanayotokana na tamaduni, pamoja na mifumo ya kiupelelezi kwa jeshi la polisi.

Akihutubia katika sherehe hizo katibu wa CCM wilayani Bunda Mobutu Malima, ametoa wito kwa wananchi wa kata hiyo ambao wengi wao ni wafugaji kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kuondokana na changamoto hiyo.

Aidha kutokana na changamoto hiyo ya upungufu wa vyumba vya madarasa katika shule hiyo katibu huyo wa CCM wilayani Bunda, aliamua kuanzisha harambee katika sherehe hiyo, ambapo zilipatikana zaidi ya shilingi milioni mbili, mifuko 43 ya saruji, ng’ombe watatu na kondoo mmoja.

Mwenyekiti wa CCM wilayani Bunda Justin Rukaka, amewataka wanachama wa chama hicho wilayani humo, kuwa mstari wa mbele na kuwa mfano wa kuigwa katika kuchangia miradi ya maendeleo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad