Siku moja baada ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole, kudai hatua ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kufanya mikutano ya hadhara ni ukorofi na uvunjifu wa sheria, uongozi wa chama hicho cha upinzani umemjibu, ukidai kauli yake hiyo ni ya watu wasiopenda kufikiri.
Wiki iliyopita, Chadema kupitia Katibu Mkuu wake, Dk. Vicent Mashinji, ilitangaza kuwa inatarajia kuanza mikutano ya hadhara baada ya kukamilisha mambo yake ya ndani.
Chama hicho kilieleza kuwa kinatambua kuwapo kwa zuio la serikali kufanya maandamano na mikutano ya siasa nchini, lakini kitaendesha mikutano hiyo kwa kuwa iko kisheria na kwamba CCM wamekuwa wakiifanya bila kuchukuliwa hatua.
Baada ya Chadema kutangaza uamuzi huo huku wakiitaja CCM kukiuka agizo la Rais John Magufuli la Juni 23, 2016, ya kuzuia mikutano ya siasa na maandamano, Polepole alizungumza na gazeti la Nipashe kuhusu kauli hiyo na kudai chama hicho cha upinzani kutangaza kufanya mikutano nchi nzima, ni ukorofi na uvunjifu wa sheria.
Akijibu kauli hiyo ya Polepole jana, Dk. Mashinji, alidai kauli ya Polepole ni ya mtu mvuvi ambaye anapinga kitu bila ya kuwa na hoja.
"Hiyo ni kauli ya watu wavivu ambao hawapendi kuzihangaisha akili zao kupinga hoja zinazotolewa," Dk. Mashinji alisema, "kufanya mikutano ni uvunjifu wa sheria? Hebu atuambie ni sheria au kanuni ipi anayozungumzia hapo ambayo inakataza mikutano.
"Hawa ndiyo vijana wa CCM ambao wamepewa nafasi bila kuandaliwa, hawajui wazungumze nini. Sisi tutaendelea na programu zetu za mikutano kama tulivyoeleza awali.
"Polisi wetu hawana shida, tunawaandikia barua kuwataarifu kuhusu mikutano yetu, wanakuja wanatulinda, hawana shida na sisi. Sasa huyu Polepole anazungumzia sheria ipi au kuna kanuni ipi inayozuia mikutano?"