Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetangaza kuanza mikutano ya hadhara mchana kweupe na kwamba kwa sasa kinachofanyika ni kufanya utaratibu na utengenezaji wa ratiba wapi itakapoanzia.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Vicent Mashinji, amesema hayo leo wakati Chadema kikitoa maazimio ya kikao maalum cha Kamati Kuu iliyokutana kwa siku mbili jijini Dar es Salaam kuanzia Februari 9.
"Kufanya mikutano ya hadhara siyo jinai na hata aliyezuia aliizuia kwa utashi lakini siyo kwa msukumo wa kisheria. Ni kweli hata sisi tulikuwa na mambo ya ujenzi wa taasisi kwa hiyo hatukuwa na uwezo wa kufanya vitu viwili kwa wakati mmoja;
"Kufanya mikutano ya hadhara, kukimbizana na chaguzi zetu za ndani, kukimbizana na majukumu ya kiutawala za uchaguzi ndio maana agizo la kuzuia mikutano ya hadhara lilipotoka imeonekana kana kwamba tumetii amri isiyo halali," amesema na kuongeza;
"Wanatumia kivuli kuwa Chadema inakwenda kufanya mikutano ya hadhara kutukana , hatuna muda huo mchafu, tuna sera zetu ambazo wananchi wanatakiwa kuzitambua."