KWA sasa klabu ya soka ya Simba itakuwa ni bandika bandua mpaka kieleweke ili kwenda sawa na timu nyigine kwenye Ligi Kuu pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kwa sasa Simba imeanza maandalizi ya mchezo wake wa ligi dhidi ya watani zao Yanga, ambao utapigwa Jumamosi, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Baada ya hapo ni safari Jumapili Arusha ambapo itafanya mazoezi kwa siku moja kabla ya mechi yake dhidi ya African Lyon itakayopigwa tarehe 19 Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Itarejea Dar es salaam na kujianda kwa siku moja kisha tarehe 22 itamenyana na Azam FC na kusafiri kwenda Iringa na itakuwa na siku mbili za mazoezi ambapo itacheza tarehe 26 dhidi ya Lipuli FC.
Baada ya mchezo huo itaunganisha Shinyanga na itakuwa na siku mbili tu za mazoezi kabla ya Machi 3 kuivaa Stand United ambapo baadaye itarudi Dar es Salaam kwa ajili ya maandalizi ya safari ya kwenda Algeria Machi 6 kwenda kucheza na JS Saoura Machi 9.
Simba inashika nafasi ya pili kwenye Kundi D ikiwa na alama sita nyuma ya Al Ahly yenye alama saba huku JS Saoura wakishika nafasi ya tatu wakiwa na alama tano na AS VIta wakishika mkia wakiwa na alama nne.