Mkuu wa wilaya ya Arumeru, Mhe. Jerry Muro, amewataka Maafisa watendaji wa kata na vijiji wilayani humo, kufanya kazi kwa bidii kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma, kwa kuweka mbele maslahi ya taifa ya kuwahudumia wananchi katika maeneo yao.
Mkuu huyo wa wilaya ametoa rai hiyo, wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha maafisa tarafa na Maafisa watendaji wa kata na vijiji wa halmashauri zote mbili za wilaya ya Arumeru, chenye lengo la kuwakumbusha na kuwajengea uwezo watalamu hao katika kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano halmashauri ya Arusha.
Amesema, kama wilaya wamemekubaliana kuanzisha programu maalumu ya mafunzo kwa watendaji hao, kwa kushirikiana na chuo kilichopo ndani ya wilaya hiyo, chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru, baada ya kugundua uhitaji wa mafunzo kwa watalamu hao, mafunzo yatakayowawezesha kuwa na uelewa wa pamoja katika kuteleleza majukumu yao.
Amesema kuwa Maafisa hao huajiriwa kutoka kwenye kada tofauti, jambo ambalo wakati mwingine, linalopelekea changamoto ya kukwamisha baadhi ya kazi, kupitia mafunzo hayo yatawawezesha kuwa na uelewa wa pamoja na kufahamu majukumu yao na mipaka ya kazi yao, kufanya kazi kwa uadilifu, kujiamini, kuongeza ari na morari ya kazi, pamoja na kuweka mbele uzalendo kwa maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla.
"Tumegundua kuna umuhimu kupata mafunzo kwa watendaji wote, yatakayowakumbusha na kuwawezesha kutambua namna sahihi ya utekelezaji wa kazi zenu za kila siku, hii imetokana na baadhi ya watendaji kushindwa kutekeleza majukumu yenu kwa usahihi na kusababisha malalamiko mengi kwa wananchi" amesema Mkuu huyo wa wilaya.8
Hata hivyo Mhe. Muro amewasisitiza watendaji hao kusimamia hali ya usalama katika maeneo yao, kwa kutambua wageni wanaoingia na kutoka katika maeneo yao, kuhamasisha wananchi kushiriki kuchangia maendeleo katika maeneo yao, huku kipaombele kikiwa ni ujenzi wa vyumba vya madarasa hususani kwenye shule za sekondari, lengo likiwa ni kuunga mkono jitihada za serekali la kutoa elimu bila maliopo linalotoa fursa ya kila mtoto kupata nafasi ya kusoma mpaka kidato cha nne.
"Kazi kubwa ya mwaka huu ni kujenga vyumba vya madarasa, ninawaomba Maafisa Watendaji, tuelekeze nguvu zetu kuhamasisha jamii kujikita katika kujenga madarasa, nataka nione kila Tarafa ina shule ya kidato cha 5-6 na kila kata ya kidato cha 1-4" amesema Mhe. Muro
Kwa upande wao wakurugenzi wa halmashauri zote mbili, wamewataka Maafisa Watendaji hao kusimamia shughuli za maendeleo kwa kuendana na kasi ya serikali iliyopo madarakani,serikali ya awamu ya tano, kuwa waadilifu katika kutekeleza kazi zao, kutoa huduma sawa kwa wananchi na kusimamia haki, na kuongeza kuwa hawatosita kuwachukulia hatua wale wote watakaofanya kazi kinyume na maadili.
Kikao kazi hicho, kiliambatana na mafunzo yaliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya Jamii kutoka chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru, Mkufunzi Douglas Mwadolago, mafunzo yaliyolenga kuwajengea uwezo watendaji hao ya mbinu bora za kuhamasisha jamii, kushiriki katika shughuli za maendeleo katika maeneo yao.
Hata hivyo watendaji hao, wamesifu juhudi zinazofanywa na halmashauri zao kupitia ofisi ya mkuu wa wilaya, na kusema kuwa mafunzo hayo yanawaongezea ujuzi na maarifa zaidi ya kutekeleza kazi zao na kuahidi kwenda kutumia maarifa waliyoyapata katika kazi zao za kila siku.
Afisa Mtendaji wa kijiji cha Kikuletwa kata ya Mbuguni, halmashauri ya Meru, Flora Maghimbi amesema kuwa, amefurahishwa na mafunzo hayo na kuahidi kwenda kuyafanyia kazi, huku akiahidi pia kutekeleza maagizo yaliyotolewa kwa kuwa yote yanalenga maslahi ya jamii wanayoihudumia.
Awali, Wilaya ya Arumeru inaundwa na halmashauri mbili, halmashauri ya Arusha na Meru, ikiwa na jumla ya Tarafa 6, kata 53 na vijiji193
DC Jerry Muro Awafunda Maafisa Tarafa Watendaji Wa Kata Na Vijiji
0
February 02, 2019
Tags