Deni la Taifa Lazidi Kukua Lafikia Shilingi Trilioni 61.8
0
February 03, 2019
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imebaini kuwa deni la taifa limekua kukua kutoka shilingi trilioni hamsini na tatu nukta tatu mwaka 2017 hadi shilingi trilioni sitini na moja nukta nane mwaka 2018 kutokana na mahitaji ya uwekezaji kwenye miradi ya maendeleo na kijamii nchini kwa ajili ya kukuza uchumi.
Akizungumza bungeni jana wakati akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo katika kipindi cha nusu ya mwaka 2018/19, mwenyekiti wake, George Simbachawene alisema, “Kwa sasa Serikali imelazimika kujielekeza kukopa mikopo yenye masharti ya kibisahara (non concessional loans) kuliko yenye masharti nafuu (concessional) kama ilivyokuwa awali.
“Kamati inaona mikopo hiyo ina riba kubwa na hivyo kuwepo kwa mzigo mkubwa wa ugharamiaji wa mikopo kupitia mapato ya ndani.”
Simbachawene alisema hadi Novemba mwaka jana, Deni la Taifa lilikuwa Sh61.8 trilioni ambazo zimetokana na ukuaji wa deni hilo kwa taratibu kutokana na uwekezaji kwenye miradi ya maendeleo na kijamii nchini kwa ajili ya kukuza uchumi.
Alisema deni la Serikali linaendelea kukua likijumlisha fedha zilizokopwa kutoka vyanzo vya ndani na nje na sekta binafsi kwa ajili ya kugharamia miradi.
“Kamati inatambua kuwa Serikali hukopa kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kupata fedha za kigeni na kukopesha taasisi za ndani za umma kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kimkakati,” alisema.
Mbunge huyo wa Kibakwe alisema kutokana na sababu nzuri za ukopaji ikiwamo uhimilivu wa deni, bado kamati yao inashauri Serikali iangalie uwiano uliopo kati ya mwenendo wa upatikanaji wa mapato ya ndani pamoja na ulipaji wa deni la Serikali na athari zake katika bajeti a uchumi.
Kamati hiyo ilishauri kuwa, umefika wakati Serikali ipange bajeti yake ya maendeleo kwa kutegemea mapato yake ya ndani na mikopo ya ndani ambayo upatikanaji wake ni wa uhakika.
Aliitaka Serikali kuhakikisha kuwa ukopaji wake katika vyanzo vya ndani hauathiri upatikanaji wa mikopo kwa sekta binafsi huku akiipongeza kwa kuendelea kufanyia kazi mapendekezo mbalimbali yanayotolewa na kamati hiyo.
Simbachawene alisema hadi Desemba mwaka jana, Serikali ilikuwa imekusanya Sh12.8 trilioni sawa na asilimia 80.4 ya lengo la kukusanya Sh15.974 trilioni na asilimia 32.5 ya lengo la mwaka ambapo zinatakiwa kukusanywa Sh32.475trilioni.
Alisema kodi ya ushuru wa forodha inaongoza kwa kukusanya Sh3.143 trilioni ikifuatiwa na walipa kodi wakubwa waliokusanya Sh2.980 trilioni wakifuatiwa na kodi za ndani Sh 1.594trilioni.
Alitaja sababu ya kutofikiwa kwa lengo la nusu mwaka kuwa ni kutokana na kutopokewa kwa misaada kwa wakati ambapo hadi kufikia Desemba mwaka jana, kiasi kilichokuwa kimepokewa na Serikali kutoka nchi wahisani ilikuwa ni Sh878.8 bilioni kati ya Sh 2.676 trilioni zilizoahidiwa.
Alisema kati ya Sh12.839 trilioni zilizokusanywa, Sh4.77trilioni sawa na asilimia 37.1 zilitumika kugharamia Deni la Taifa pamoja na riba ya madeni yaliyoiva ambapo Sh3.311 trilioni zilitumika kulipa mishahara na Sh4.749 trilioni ndizo zilizotumika kwa shughuli za maendeleo.
Alisema kwa mwendo huo, huenda Serikali ikashindwa kufikia malengo yake ya makusanyo kwani inaonyesha inaweza kufikia asilimia 80 hadi 95 na kupendekeza iongeze wigo wa ukusanyaji mapato ya ndani na kutafuta vyanzo vipya vya mapato.
Tags