Diamond Hutopata Baba Mzazi Mwingine, Epuka Hii Laana
1
February 26, 2019
NIMESHITUSHWA sana na hali aliyofikia mzazi wa msanii Diamond. Namzungumzia Abdul Juma anayesumbuliwa na matatizo ya miguu yake ambayo imevimba na kuwa na sura inayoogopesha kutokana na maradhi.
Kwa wale waliofanikiwa kuona picha za miguu yake na hali iliyofikia ni kitu kinachosikitisha sana. Naweza kuwa wazi moja kwa moja kwamba mzazi yule hapaswi kuteseka vile. Vyovyote inawezekana, unajua wazazi ni wanadamu ndiyo maana hata Nassibu Abdul naye ni mzazi kwa sasa. Anaweza akawa hakuwahi kuwakosea watoto wake lakini kuna siku anaweza kufanya kosa.
Uwezekano wa Baba Diamond kuwa na makosa au kosa kubwa alilowahi kulifanya kwa mwanaye upo, lakini pia Diamond akaamua kunyamaza kutotaka kulizungumzia katika jamii. Bahati mbaya, uhalisia unaonyesha hivi; baba Diamond anateseka kutokana na kuugua na hali yake si nzuri kwa kuwa akiendelea hivyo, siku moja anaweza kuangukia sehemu ambayo si sahihi.
Kama ni hivyo, Diamond kama mwanadamu anayeamini wanadamu hukosea, kama ni mwanadamu anayeamini kuna Mungu kupitia mafunzo yake ya dini amesisitiza suala la msamaha kama ambavyo yeye Diamond amekuwa akimkosea Mungu na akaendelea kuomba msamaha halafu siku nyingine akakosea tena.
Mfano, baba yake awe aliwahi kumfukuza yeye na mama yake, halafu akatafuta mwanamke mwingine na kuanza kuishi naye kwa raha mustarehe huku yeye Diamond na mama yake wakiteseka, hakika ni maumivu lakini bado haitazuia msamaha.
Nikuambie kitu, kama inatokea mtu anakufanyia maudhi hadi inafikia hatua ya kuapa hutamsamehe, wakati mwingine unapaswa kumshukuru. Nitakuambia kwa nini; maana watu wenye maudhi ni walimu wanaotoa mafunzo ya ukomavu kuliko hata yale ya jeshini.
Kama utakuwa na ndugu au mzazi ambaye anakulea kama yai huku akitaka usiguswe au kuumizwa, mara nyingi unaishia kuwa lainilaini kwa kuwa haukuwa na sababu ya msingi kugangamala au kutaka upambane.
Yule anayekuibulia timbwili kila mara, anaudhi na kuumiza lakini utakubaliana nami huwa anaamsha akili yako ambayo haukuwahi hata kufikiria kama unayo nyingi kiasi hicho. Wakati akili inaanza kuamka huwa kuna mateso, maumivu na uchungu wa kuumizwa au kutengwa. Mwisho wa wengi umekuwa mzuri na mafanikio kuliko hata wale waliowaumiza.
Vizuri ukajifunza hapa. Mimi huwa naona watu wa aina hii huwa ni kama vile “wametumwa na Mungu” ili kukuamsha na kukuonyesha utumie uwezo wako kwa kiasi sahihi kuliko kutulia ukiendelea kupata kila unachotaka.
Pointi yangu hapa ni hivi; inawezekana mzee Nassibu aliwahi kumpa mwanaye mateso makubwa. Lakini ndiye akawa msaada wa kumuibua kwa kuwa ilikuwa lazima Diamond apambane kufikia hapa ili aweze kujikomboa mwenyewe na mama yake Bi Sandra.
Mwisho namuombea Bi Sandra, inawezekana kabisa pia naye aliudhiwa sana na mzee Nassibu, huenda kwa matatizo kadha wa kadha enzi zao. Pamoja na hivyo ana nafasi ya kumrudisha Diamond kwa mzee wake. Hata kama hakutakuwa na ukaribu upya unaofanana na zamani, basi hata kumhudumia tu kama ambavyo amewahi kujitolea kwa wengine.
Aliwahi kumzawadia gari Mzee Gurumo (Mwenyezi Mungu amrehemu). Alimsafirisha Hawa hadi India kwenda kutibiwa, vipi ishindikane kwa mzee wake na Bi Sandra ukiwa kimya.
Hata kama bado una uchungu kama kweli kuna matatizo yalitokea huko nyuma, kumbuka Diamond hawezi kupata baba mzazi mwingine na mwisho, mali zake hazitakuwa na thamani kwake kama hakuwahi kumsaidia mzazi wake ikafikia akakatwa miguu.
Ukishindwa kuokoa miguu ya baba yako, gari au nyumba ya fahari ya nini sasa? Bi Sandra, msaidie Diamond kwa kumpunguza hasira amsaidie mzee wake na kama wewe huwa unazijaza, basi punguza kasi ya pampu yako ili amsaidie mzazi wake. Sisi zote, si wakamilifu.
I salute your comment, Ushauri wako ni mzuri sana, mzazi ni mzazi tuu huwezi kumbadilisha hata awe mbaya vipi! Mtoto hawezi kumhukumu mzazi, ni Mwenyezi Mungu tu wa kuhukumu. So kijana Diamond mrejee Mungu wako ndie aliekupa na ndie alie wanyima wengine kwa hekma yake.
ReplyDelete