Mwanamuziki mkongwe wa bongo Fleva, Hafsa Kazinja ambaye kwa sasa ameokoka, amesimulia yaliyomtokea kwenye maisha yake, mpaka kuamua kumkabidhi Yesu nafsi yake.
Akielezea simulizi hiyo yenye kutisha iliyojaa matukio ya kichawi, Hafsa amesema kwamba kabla hajaokoka aliumwa kwa zaidi ya miaka 6, na kuamua kukimbilia kwa waganga wa kienyeji, jambo ambalo likamuongezea matatizo zaidi.
Ameendelea kusimulia mkasa huo akisema kwamba mwanzo alikuwa akiona vitu vya ajabu ikiwemo majoka makubwa yakiwa jukwaani yakicheza pindi anapofanya show, huku akisikia sauti za kunguru wakilia hata kama yuko mbali nao, na kumfanya ashindwe hata kujichangaya na watu, akiishia kujifungia ndani peke yake. Baadaye ndipo alipokata shauri la kutafuta suluhu kwa waganga wa kienyeji, ambao walimwambia kuwa majini yanamtaka yeye awe mganga wa kienyeji.
“Mwaka 2008 nilianza kupata matatizo, ilifika wakati nikawa naona vitu vya ajabu, majoka, majitu makubwa, naona majoka makubwa yanakwenda kwenda tu, mchana, usiku, unaweza ukawa unaongea na mimi nikawa 'naconcetrate' kuangala ninavyoviona, nilibadilika nikawa sipendi kuongea na watu, nikawa najifungia ndani, hata nikiwa stejini naona majoka kama ndio mastage show”, amesema Hafsa.
“Nikaanza kwenda kwa waganga kwa ajili ya kutafuta uponyaji, kuna nyumba yangu nilikua najenga, nikauza, nikawa baada ya kupona ndio nazidiwa, niwe macho au nimelala naona vitu vya ajabu, nikapoteza nyumba, magari matatu”.
Akiendelea kusimulia hayo Hafsa akasema kwamba, "niliingia ndani zaidi, wengine wananiambia ni mizimu, wengine wakawa wananiambia unatakiwa uwe mganga, nikaenda Bukoba nikajengewa mpaka vizimba vile, nikawa najiuliza nakuwaje mganga!. Nikawekewa masharti kila nikipata pesa nikatoe kama sadaka, nimepigwa sana nyungu, nimehangaika sana”, amesea Hafsa.
Akienda mbali zaidi na kusimulia jinsi alivyofunguliwa, Hafsa ansema siku hiyo alikwenda kwa mganga na kunyweshwa damu ya kuku, kisha akasikia sauti za watu wakimtukana Mungu, ndipo ufahamu ulipomjia na kuamua kubadilika mpaka kuokoka.
“Nilivyouza gari ya mwisho ili nifanyiwe hayo majini yanavyotaka, alichinjwa kuku, akachukua damu akanipa ninywe, nikanywa, pale pale nikasikia sauti watu wanamtukana Mungu, ingawa nilikuwa nakwenda kwa waganga ila nilikuwa nasali, nikapata ufahamu ikiwa wanamtukana Mungu, nitakimbilia wapi siku nikifa, nilimchukia mganga, nikachukia na waganga ndipo nikapata msaada kwa mtu kunipeleka kanisani na kuokoka, na mpaka sasa ndio nipo huko na nimepona kabisa”, amesema Hafsa.
Hivi sasa msanii huyo amefunguka kuwa anaimba muziki wa injili, na sio bongo fleva tena.