Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amezungumzia taarifa ya kuhojiwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad pamoja na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee.
Akizungumza jana jijini Dodoma kabla ya Mkutano wa Kumi na Nne wa Bunge kuahirishwa, Spika Ndugai alisema kuwa taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge baada ya kuwahoji kwa nyakati tofauti CAG na Mdee itatolewa katika Bunge lijalo kutokana na ufinyu wa muda.
“Waheshimiwa wabunge taarifa za Kamati ya maadili ziko tayari lakini tunakosa muda kama mnavyoona wenyewe, tutazileta katika mkutano ujao,” alisema Spika Ndugai.
Aidha, Ndugai amefafanua kuwa hana tatizo na watu kulikosoa Bunge lakini angependa kuona kuna kushauriana na kusaidiana badala ya kudharauliana.
Januari 21 mwaka huu, baada ya mijadala mingi na kufunguliwa kwa kesi ya kikatiba kuomba Mahakama kutoa tafsiri ya Ibara inayozungumzia madaraka ya CAG, Kamati ya Bunge ilimhoji na siku iliyofuata ikakamilisha kwa kumhoji pia Mdee.
CAG alihojiwa kutokana na kauli yake aliyoitoa alipokuwa nchini Marekani akizungumza na chombo cha habari cha Umoja wa Mataifa ambapo alisema kuwa “kama Bunge halizifanyii kazi ripoti zake huo ni udhaifu wa Bunge.”
Spika Ndugai alilaani vikali kauli hiyo na kumtaka kufika mbele ya Kamati ya Bunge Januari 21 vinginevyo angefuatwa kwa pingu.