KOCHA Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, leo Jumamosi anaweza kuwashangaza wengi kwa namna ambavyo atapanga kikosi chake cha kwanza kuna uwezekano mshambuliaji tegemeo timu hiyo, Emmanuel Okwi, akianzia benchi.
Sapraizi hiyo anaweza kuifanya Aussems kutokana na aina ya mazoezi ya mwisho aliyowapa wachezaji wake jana Ijumaa kwenye Uwanja wa Boko uliopo Ununio, Dar.
Imezoeleka kuwa, Okwi anapokuwa fiti, huwa anaanza kikosi cha kwanza hasa kwenye mechi nyingi ngumu, lakini leo Jumamosi kwenye mchezo huo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar ambao Yanga ni wenyeji, Okwi anaweza kuanzia benchi akiwaacha John Bocco na Meddie Kagere wakianza.
Championi ambalo jana lilikuwepo mazoezini hapo, lilimshuhudia Okwi akifanyishwa mazoezi maalum peke yake kwa kunyonga baiskeli maalum ya mazoezi huku wenzake wakiendelea na mazoezi ya pamoja.
Hata lilipofika zoezi la kufunga mabao, Okwi aliendelea na zoezi lake hilo hali ambayo inaonyesha dhahiri ana hatihati kuanza kikosi cha kwanza. Wakati Okwi akiwa na hatihati hiyo, beki kisiki, Juuko Murshid, jana alifanya mazoezi huku kwenye ugoko wake kukiwa na kifaa maalum cha kuzuia asijitoneshe jeraha lake la ugoko.
Juuko aliyetajwa kuwa kwenye hatihati ya kucheza mechi ya leo, jana alifanya mazoezi ya pamoja na wenzake huku kocha akimpanga kwenye safu ya ulinzi sambamba na Pascal Wawa akiwafundisha namna ya kuwazuia wapinzani. Akizungumzia mazoezi hayo ya mwisho kuelekea mechi ya leo, Aussems alisema: “Tumemaliza salama mazoezi, kilichobaki ni kusubiri wakati ufike, mechi ichezwe.
“Katika mchezo huu, kikosi changu kitakuwa na mabadiliko kidogo kutokana na masuala ya kiufundi ambayo siwezi kuyasema kwa sasa.”
Licha ya Aussems kusema kutakuwa na mabadiliko kwenye kikosi chake cha leo, lakini kuna uwezekano mkubwa wa kikosi hicho kikawa hivi; Aishi Manula, Zana Coulibaly, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Juuko Murshid, Pascal Wawa, James Kotei, Clatous Chama, Jonas Mkude, John Bocco, Meddie Kagere na Hassan Dilunga.
Hiki Hapa Kikosi Cha Simba Kitakachoivaana na Yanga
0
February 16, 2019
Tags