Wafanyabiashara wa Dawa za kulevya aina ya Mirungi wamebuni mbinu mpya za kusafirisha dawa hizo kwa kutumia magari ya Kifahari yakiwemo Toyota Land Cruser ,Toyota Alphasad,Toyota Vanguard huku wengine wakilazimka kuzifanyia mabadiliko gari aina ya Toyota Noah ili kurahisisha ubebaji wa Mirungi kwa kificho.
Jeshi la Polisi mkoa wa Kilimanjaro limebaini mbinu hizo baada ya kufanikiwa kukamata gari aina ya Toyota Noah lenye namba za usajili T 443 DET lililokuwa limebeba kilogramu 102 za Mirungi likielekea Kondoa mkoani Dodoma.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Hamis Issah alithibitisha kukamatwa kwa gari hilo majira ya saa 6:30 za usiku katika kizuizi cha askari eneo la Kwa Wasomali likielekea njia ya Arusha.
“Tumeendelea na zoezi la kukamata wasafirishaji wa Dawa za kulevya, tumekamata kwa mara nyingine gari aina ya Noah, hili gari limetokea maeneo ya mkoani Kilimanjaro ,linaelekea mkoani Dodoma katika wilaya ya Kondoa “alisema Kamanda Issah
Alisema hadi sasa watu wawili wanashikiliwa huku akiwataja majina kuwa ni Simoni Boa mkazi wa Babati na aliyekuwa dereva wa gari hilo na Abushil Abdalah mkazi wa Kondoa na kwamba taratibu zikikamilika watafikishwa mahakamani huku akitoa onyo kwa wafanyabiashara wa Mirungi walioshindwa kuacha biashara hiyo .