Jifunze Hili Fundisho la Mapenzi Kutoka Kwa Obama na Rais Putin Aliyekimbiwa na Mkewe

ADIMIR Putin ni kati ya wanaume wachache ambao wana kila kitu duniani. Hata hivyo, maisha yake ya kimapenzi yaliingia doa mwaka 2013 baada ya aliyekuwa mke wake, Lyudmila Putina kung’ang’aniza talaka.

Zingatia, taasisi nyingi za utafiti zilimtaja Putin ambaye ni Rais wa Urusi kuwa ndiye alikuwa binadamu mwenye nguvu kuliko wote duniani kwa mwaka 2016. Putin ana fedha nyingi na mamlaka makubwa. Anaongoza taifa kubwa.

Pamoja na tuhuma kwamba Putin alikosa uaminifu kwa kuchepuka nje ya ndoa na mwanamichezo mshindi wa medali ya dhahabu Olimpiki, Alina Kabaeva, kilichoelezwa na Lyudmila ni kuwa maisha ya ndoa yalikuwa magumu na alikuwa mpweke kwa sababu Putin hakuwa akitulia nyumbani.

Ndoa ya Lyudmila na Putin ilidumu kwa miaka 20. Hata hivyo, Lyudmila aliona ‘miguvu’ ya Putin haina faida, alimchoka na kulazimisha waachane kisha kuuacha ‘u-first lad’ wa Urusi. Hivyo, tambua kuwa hata ujione maalum kiasi gani kama humfai mwenzako kimapenzi mtaachana tu.

Chukua mfano wa Michelle Obama jinsi alivyokuwa mke wa Rais mwenye furaha kipindi chote mume wake akiwa Rais wa Marekani. Obama hakujiona kuwa yeye ni zawadi inayoliliwa na wengi, badala yake alijionesha mbele za watu kwamba hakuna yeye bila mkewe na watoto wake, Malia na Sasha.

Siku zote usiache kufahamu kuwa ukiwa kiongozi, tajiri au mtu maarufu ambaye unajichukulia kuwa wewe ni maalum, utajikuta unamtengeneza Lyudmila kwenye maisha yako ya kimapenzi na matokeo yake ataomba kuachika.

Ukiwa ni kiongozi, tajiri au mtu maarufu ambaye unatoa kipaumbele kwa mwenzi wako, utamtengeneza Michelle Obama wako. Na hiyo ni pande zote mbili, mume na mke. Hakuna ambaye ana ruhusa ya kujigeuza mkubwa kwenye mapenzi dhidi ya mwenzake.

Mapenzi ni zawadi inayoingia na kutoka. Kwamba wewe ni zawadi ya mwenzako, naye ni zawadi yako. Haipaswi kuwa mmoja ajione zawadi kisha amwone mwenzake kama aliyebahatika kupata zawadi.

Unakuta watu ni wapenzi lakini mmoja anamilikiwa mwingine hamilikiwi. Mapenzi yanatakiwa kuonekana kila mmoja anammiliki mwenzake. Kila mmoja awe na uwezo wa kumdhibiti mwenzake. Siyo mmoja anakuwa mtoa amri na mwingine mtekelezaji tu.

Ndimi Luqman MALOTO

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad