Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Yafunguka sakata la ufisadi wa Sh1.5 trilioni

Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Yafunguka sakata la ufisadi wa Sh1.5 trilioni
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imesema uhakiki uliofanywa kuhusu sakata la ufisadi wa  Sh1.5 trilioni katika mfuko mkuu wa Serikali umebaini kuwa hakuna tofauti  ya makusanyo na mapato ya Serikali katika Mfuko Mkuu kwa mwaka wa fedha 2016/17.

Hayo yameelezwa leo bungeni jijini Dodoma na mwenyekiti wa kamati hiyo, Nagenjwa Kaboyoka wakati akiwasilisha taarifa ya PAC kwa mwaka unaoishia Juni 30, 2018.

Amesema hilo lilibainika baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalum katika mfuko mkuu.

“Kamati ilibaini kuwa hakuna fedha yeyote katika Mfuko Mkuu ilikuwa imepotea. Hii imethibitishwa na maelezo CAG kama alivyonukuliwa,” amesema Kaboyoka.

Sakata la fedha hizo liliibuliwa na mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe alipokuwa akichambua ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG ) ya 2016/17 alipozungumza na waandishi wa habari Aprili, 2018.

Sakata hilo ambalo tangu lilipoibuliwa na mbunge huyo na kuibukia bungeni katika mikutano ya Bunge, Serikali imeendelea kusema italitolea ufafanuzi katika kamati ya PAC.

Suala la fedha hizo ambazo Zitto alidai hazionekani jinsi zilivyotumika katika ripoti ya CAG, lilipata ufafanuzi Aprili 20, mwaka jana wakati Rais John Magufuli akiwaapisha majaji wapya Ikulu jijini Dodoma.

Rais Magufuli alisema hakuna fedha iliyoliwa na kama ingekuwa hivyo, basi watendaji waliohusika angewachukuliwa hatua.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad