Katibu Mkuu CCM Dkt. Bashiru Ally Amvaa Tundu Lissu

Katibu Mkuu CCM Dkt. Bashiru Ally Amvaa Tundu Lissu
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Bashiru Ally amemtaka Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) kuacha kutoa matamshi yanayoichafua Serikali na vyombo vya usalama na kumualika kujiunga na chama hicho kama ameshindwa kufundwa kisiasa aliko.

Dkt. Bashiru ameyasema hayo alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa ndani wa chama chake, ambapo alilaani kauli zilizotolewa na Lissu kuhusu tukio lake la kushambuliwa kwa risasi na jinsi anavyovihusisha vyombo vya usalama na Serikali.

“Kama amechoka kwenye chama kisichokuwa na itikadi aje CCM. Afundwe, afundishwe namna ya kuwasiliana na umma, namna ya kuchagua maneno, namna ya kuheshimu Mamlaka, namna ya kupenda nchi yako,” alisema Dkt. Bashiru.

“Haifai, kiongozi anayetaka kuwa Rais wa nchi hii kuwa na matamshi ambayo hayachagui na haangalii athari zake. Kazi yetu ni kuchapa kazi, ataumbuka,” aliongeza.

Aidha, Katibu huyo wa CCM alitoa mifano ya matukio ya kiusalama na ajali zilizowahi kuwapata viongozi wa kitaifa awali, akieleza kuwa matukio hayo pamoja na ukubwa wake hayakuitikisa nchi na kuichafua.

Alisema kuwa Lissu anasema alipigwa risasi ‘mchana kweupe’, matukio mengine kama yake dhidi ya viongozi wa Serikali na wanausalama yalifanyika hadharani kweupe.

“Anasema alishambuliwa mchana kweupe, hata marehemu [Edward] Sokoine alipata ajali mchana kweupe. Askari wetu kule Rufiji waliuawa mchana kweupe. Na matukio ya namna hiyo yanandelea mchana kweupe. Na wote wana thamani ileile ya uhai. Naomba kutumia wasaa huu kuwakumbusha wanasiasa kuwajibika na matamshi yao na kuacha ubinafsi,” alisema Dkt. Bashiru.

Katibu huyo wa CCM alisema kuwa vyombo vya ulinzi na usalama nchini vinafanya kazi kubwa ya kulinda usalama na ndani ya nchi na mipaka yake na vimepata heshima tangu kupatikana kwa uhuru

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad