Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Simon Sirro, amewasili mkoani Simiyu na kusisitiza kuwa jeshi lake liko tayari kukomesha mauaji ya watoto yanayoendelea mkoani humo.
Mataukio ya mauaji ya watoto na wanawake mkoani humo katika Kata ya Lamadi, yalianza kujitokeza wiki iliyopita ambapo zaidi ya watoto watatu wameshauawa.
IGP Sirro ambaye aliwasili leo Jumatatu Februari 18, saa nne asubuhi na kupokelewa na Mkuu wa Upelelezi Mkoa, Benjamini Kuzenza na maofisa wengine wa polisi kisha kufanya kikao cha ndani na maofisa wa jeshi hilo mkoa, kikao mbacho kilidumu kwa muda wa saa mbili.
Mara baada ya kikao hicho Mkuu huyo wa Polisi nchini alikutana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa.
Akizungumza katika kikao hicho, IGP Sirro aliwahakikishia viongozi wa Mkoa wa Simiyu kumaliza matukio ya mauaji yanayoendelea katika Kata ya Lamadi .
“Tayari tumeongeza nguvu kutoka makao makuu ya jeshi ili kushughulikia suala la matukio ya Lamadi na mauaji hayo yatakomeshwa,” amesema.