Mahakama ya Kenya hii leo itatoa uamuzi kuhusu uhalali wa sheria inayoharamisha mapenzi kwa watu wa jinsia moja.
Chini ya sheria za Kenya, mapenzi ya jinsia moja ni hatia iliyo na hukumu ya miaka 14 gerezani.
Nchini Kenya, kama ilivyo katika mataifa mengi barani Afrika, uhusiano wa jinsia moja haukubaliki kwa jamii.
Brian na Yvonne ni wanaharakati wa kutetea haki za jamii ya watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja, pamoja na wale waliojibadilisha jinsia na hisia.
''Tunadharuliwa, tunakabiliwa na ghasia, tunaumia, tunateswa, tunakosewa. Tukienda kutafuta huduma za afya tunaangaliwa kwa dharau, tunatukanwa, tunatemewa mate, tunafanywa kama sisi sio Wakenya, na kama sisi sio Binaadamu, ni kama sisi ni viumbe wasiotoka katika dunia hii'.
Chini ya sheria za Kenya zilizoandikwa enzi za ukoloni, mapenzi ya jinsia moja yametambuliwa kama kitendo kisicho cha kawaida, na kuwekwa katika kitengo kimoja na hatia ya kufanya mapenzi na Wanyama.
Wanaharakati wanasema kwamba kuwepo kwa sheria hii kumezidisha ubaguzi, huku watu wakifurushwa kutoka nyumba walizokodisha, kunyimwa nafasi za kupata matibabu na pia kuhangaishwa na polisi, yote kwa sababu ya jinsia zao.
Aidha wanaharakati wanasema kutoelewa sheria hii kumechangia dhuluma za aina nyingi.
''Unapata, wakati mwingi mtu akisema kitu kibaya au kufanya kitu kibaya dhidi ya jamii yetu. Mtu anasema, hata Kenya hairuhusiwi, sheria inapinga, kwa sababu sio watu wengi wanaokwenda kwenye hicho kifungu cha sheria kuelewa inasema nini. Yeye amesikia tu sheria, inasema,' amefafanua Yvonne.
'Kwahivyo inawasukuma watu kuendelea kuwachukulia na kuwafanyia watu wa jamii hii vibaya. Kwasababu kuna hii fikra kwamba sheria imesema. Sasa ndio maana tumekwenda kotini hiyo sheria iondolewe kwanza, ndio sasa tuongee' ameongeza mwanaharakati huyo.
Kenya leo kuamua iwapo kuhalalisha au kuendelea kupinga mapenzi ya jinsia moja
0
February 22, 2019
Tags