Kimenuka Yanga..Kocha Zahera Atangaza Kuondoka Yanga Kama Hawatofanya Hili
0
February 24, 2019
Kocha Mkuu wa Yanga, Mkongoman, Mwinyi Zahera.
KOCHA Mkuu wa Yanga, Mkongoman, Mwinyi Zahera ameweka msisitizo kuwa anaweza kuacha kazi Mei, mwaka huu kama hatopewa dola milioni 2 (Sh bil 4.6) kwa ajili ya usajili wa msimu mpya wa Ligi Kuu Bara. Mpaka sasa wakati anatishia kutimka, Zahera ameiongoza Yanga kucheza mechi 25 za Ligi Kuu Bara na kushinda 19, sare nne na mbili amepoteza. Ubora wake ulianza kuonekana mapema tu msimu huu kutokana na kuiongoza Yanga kucheza mechi 15 za ligi bila ya kufungwa na kuwa Kocha Bora wa Mwezi mara mbili.
Kauli ya kuondoka Yanga, aliitoa jana ikiwa ni siku moja imepita tangu yatangazwe mapato yaliyopatikana kutoka kwa wanachama wa Yanga kupitia kampeni yake aliyoianzisha katika kupita kipindi kigumu cha kiuchumi walichonacho.
Yanga, kupitia mratibu wa timu hiyo, Hafidh Saleh, juzi alitangaza kupatikana Sh milioni 21.3 zilizochangwa na wanachama na mashabiki wa timu hiyo kupitia mitandao ya simu na benki ndani ya mwezi huu.
Zahera ambaye alitua Yanga Aprili mwaka jana na kuchukua mikoba ya Mzambia, George Lwandamina amekuwa mstari wa mbele kuwataka wachezaji wapambane licha ya malipo yao kuchelewa. Wakati akitua, tayari timu hiyo ilikuwa na majukumu pia ya kimataifa ambapo ilikuwa kwenye hatua ya Makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo lilimaliza nafasi ya mwisho kwenye kundi lao.
Akizungumza na Championi Jumamosi kwa lafudhi ya Kikongo, Zahera alisema kuwa upatikanaji wa fedha hizo hautafanikiwa kama wanachama watakuwa wagumu katika kuichangia timu yao hiyo inayoongoza kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara. Zahera alisema, kama mashabiki hao wataendelea na kasi hiyo ndogo ya uchangiaji, basi hatakuwa tayari kuendelea kuifundisha Yanga kwenye msimu ujao na badala yake ataondoka mwishoni mwa msimu huu ambao utakuwa mwezi Mei, mwaka huu.
Aliongeza kuwa, mashabiki wa Yanga wafahamu fedha hizo za michango zinatunzwa kwenye akaunti ya benki maalum kwa ajili ya kufanyia usajili wa usajili katika msimu ujao pekee na ili timu hiyo ifanye vizuri ni lazima ufanyike usajili bora na kisasa utakaoendana na ukubwa wa timu. “Mimi kocha Zahera, nimeamua nitaachana na Yanga ifikapo mwezi wa tano, naweza kuondoka kwa sababu nishafanya mengi sana ya kuisaidia timu na hakuna ambaye atachukia kuondoka kwangu.
“Nimewasaidia kwa vitu vingi sana. Nimekuwa nikijitolea kwa nguvu zote lakini naona kuwa hata Mungu anasema ukijisaidia na yeye atakusaidia. “Wakati mimi naisaidia Yanga, naona kama wenyewe hawapendi kuisaidia, hivyo na mimi siwezi kuendelea. Timu inafahamu bila baraka za Mungu anazotupatia tusingefika hapa tulipo, sasa ninawaambia mashabiki wote na wanachama, jukumu la kuijenga timu ni sisi wenyewe.
“Naona kama hakuna chochote kinachofanyika, kwa wiki nne tumepata Sh Mil 25. Mimi nimechangia milioni mbili ila angalia mimi siyo shabiki wala mwanachama, sasa ni sababu gani wanasema Yanga ina matajiri wengi hapa nchini. “Kwa nini katika wiki moja wakashindwa kuchangia fedha, tukifikisha dola 2,000,000 (Sh bil 4.6), basi mwezi wa tano tungeweza kununua wachezaji wakubwa na kujenga uwanja wa mazoezi.
“Kikubwa wanachotakiwa kufahamu kuwa, timu inahitaji dola milioni 2 katika kufanikisha usajili ubora utakaoendana na ubora wa Yanga, kama unavyofahamu wachezaji wote nimewakuta kasoro Boban (Haruna Moshi) ambaye nilimpendekeza katika usajili wangu wa dirisha dogo.”
Zahera anatamani kuiona Yanga inakuwa na wachezaji wazuri kama wale waliopo Simba, ili kuthibitisha hilo, hivi karibuni alipofanya mahojiano na Championi alisema: “Nikipewa nafasi ya kuchukua wachezaji wa Simba, namchukua Kagere (Meddie), Bocco (John) na Chama (Clatous).”
Usajili huo wa mabilioni anaoutaka Zahera, unaonekana kuuzidi ule wa Mwekezaji wa Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’ ambaye yeye katika msimu huu ametumia Shilingi Bilioni 1.3 katika usajili wake wa wachezaji
MARTHA MBOMA NA WILBERT MOLANDI
Tags