Kocha Mkuu wa klabu ya Biashara United, Amri Said amesema kuwa sababu iliyomfanya kuwanyang'anya simu wachezaji wake karibia na mchezo ni kuwaepusha na kuchati mara kwa mara ambako kunawaharibia umakini wa mchezo.
Ameyasema hayo baada ya timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar jana, Februari 14 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliopigwa kwenye Uwanja wa Karume mjini Musoma.
Amri Saidi amesema kuwa baada ya kujiunga na timu hiyo, aliamua kuchukua uamuzi wa kuwa anawanyang'anya simu wachezaji wake siku mbili kabla ya mchezo ili waweze kuufikiria mchezo husika, jambo ambalo limewasaidia kupata matokeo mazuri katika kila mchezo ambao alitumia mbinu hiyo.
"Wachezaji wangu mara nyingi sisi tumewaunganisha kwenye group la WhatsApp la klabu na nyinginezo kwenye simu zao, lakini mpaka saa nane usiku ukimwangalia mchezaji unamkuta yupo 'online', wapo wanachati na wanawasiliana na watu wao", amesema Amri Said.
"Kwahiyo tumeamua kila inapokaribia mechi tunawanyang'anya simu na katika mechi zote ambazo tumefanya hivyo tumepata matokeo mazuri na wachezaji wamecheza vizuri, tumegundua tukichukua simu zao, wachezaji wanatuliza akili, wanalala mapema saa 3 tu unaona kila mtu ameingia kulala", ameongeza.
Pia amezungumzia adhabu aliyopewa golikipa wa klabu hiyo, Nouridine Balora ya kufungiwa mechi 5 ni kutokana na vitendo vya utovu wa nidhamu ikiwa ni baada ya kugoma kutoa simu yake kama agizo lilivyotolewa na kocha huyo ikiwa ni katika maandalizi ya mechi.
Biashara United bado ipo mkiani mwa ligi katika nafasi ya 19, ikiwa na alama 23 baada ya kucheza michezo 25 mpaka sasa.