KUELEKEA mchezo wa watani wa jadi dhidi ya Yanga, Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems amesema kuwa kikosi chake kipo fiti na morali ya hali ya juu huku akitamka kuwa anaanza na watani wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly halafu wanafuatia Yanga.
Watani wa jadi hao wanatarajiwa kuvaana Februari 16, mwaka huu kwenye mchezo wa raundi ya pili ya Ligi Kuu Bara utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Timu hizo, katika mchezo wa raundi ya kwanza ya ligi zilitoka suluhu wakati zilipokutana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Aussems alisema kupoteza michezo miwili ya michuano ya Afrika dhidi ya AS Vita na Al Ahly, siyo sababu ya wao kupata matokeo mabaya wakati timu yake itakapocheza na Yanga.
Aussems alisema matayarisho ya mechi mbili dhidi ya Al Ahly watakayocheza nayo Februari 12, mwaka huu anayafanya kwa wakati mmoja na mchezo wao na Yanga katika kuhakikisha anapata matokeo mazuri ya pointi tatu.
Aussems alisema michezo yote miwili ina umuhimu kwao, hivyo ni lazima afanye maandalizi ya kutosha ili kufanikisha malengo yake yeye pamoja na wachezaji wake.
Aliongeza kuwa, anafurahia kuona morali ya wachezaji ikiongezeka kwa wachezaji katika kuelekea mchezo dhidi ya Al Ahly ambao wamejipanga kushinda kwa kufanyia marekebisho baadhi ya nafasi ikiwemo safu ya ulinzi na ushambuliaji.
“Kabla ya kukutana na ‘derby’ ya Simba na Yanga, tutacheza mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika na Al Ahly ambao ni mchezo mgumu kwetu unaohitaji maandalizi ya kutosha ya kuhakikisha tunafanikisha ushindi.
“Michezo hiyo yote ina umuhimu mkubwa kwa kuanzia huu na Al Ahly kabla ya kucheza na Yanga, hivyo nimepanga kufanya maandalizi ya kuelekea michezo hiyo ndani ya wakati mmoja kwa kuziboresha kila sehemu nilizoziona zina upungufu.
“Hivyo, nitaanza na Al Ahly kwanza kucheza nao kabla ya kumalizana na Yanga, mchezo ambao ni mgumu pande zote, ni mechi inayovuta hisia za watu wengi kutokana na upinzani uliopo,” alisema Aussems.
Wakati huohuo, kikosi cha Simba kinatarajiwa kuingia kambini leo Ijumaa kujiandaa na mchezo wao dhidi ya Al Ahly.
Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Simba, Cresentius Mgori amesema: “Mikakati tuliyokuwa nayo ni ileile ya kupata ushindi wa pointi tatu nyumbani, hakuna zaidi ya hicho, wachezaji wataingia kambini mara baada ya kumaliza mechi yetu dhidi ya Mwadui na tunajiandaa kupata matokeo mazuri katika mechi hiyo na ligi kwani tunahitaji kutetea ubingwa,” alisema Magori.
Kuhusu ujio wa Al Ahly, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo alisema: “Bado Al Ahly hawajatuma taarifa yoyote hadi sasa (jana) juu ya ujio wao na iwapo watatuma tutaweka wazi.”